Kumalizika mchakato wa kuuzuliwa Trump, kuendelea mgawanyiko wa kisiasa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58990-kumalizika_mchakato_wa_kuuzuliwa_trump_kuendelea_mgawanyiko_wa_kisiasa_marekani
Hatimaye baada ya miezi kadhaa ya vuta nikuvute nchini Marekani, kadhia ya kuuzuliwa rais wa nchi hiyo imemalizika baada ya Baraza la Seneti linalohodhiwa na Warepublican kumtoa hatiani Donald Trump na kufumbia macho utumiaji wake vibaya madaraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2020 21:41 UTC
  • Kumalizika mchakato wa kuuzuliwa Trump, kuendelea mgawanyiko wa kisiasa Marekani

Hatimaye baada ya miezi kadhaa ya vuta nikuvute nchini Marekani, kadhia ya kuuzuliwa rais wa nchi hiyo imemalizika baada ya Baraza la Seneti linalohodhiwa na Warepublican kumtoa hatiani Donald Trump na kufumbia macho utumiaji wake vibaya madaraka.

Kikao cha 12 cha kesi iliyokuwa ikimkabili rais wa 45 wa Marekani kilianza Februari 5 jioni kwa saa za Marekani katika Baraza la Seneti na katika siku hiyo ya mwisho ya kesi hiyo maseneta walipiga kura baada ya waungaji mkono na wapingaji wa mpango wa kumuuzulu Trump kutoa maoni yao. Katika mchakato wa upigaji kura, Baraza la Seneti, linaloongozwa na Warepublican wenzake Rais Trump, lilipiga kura ya kumuondoa hatiani kwa kura 52-48 kuhusu mashtaka ya utumiaji mbaya wa madaraka na kura 53- 47 kuhusu mashtaka ya kuzuia Bunge kufanya kazi yake. Seneta Mitt Romney wa Warepublican aliungana na Wademocrat  katika kuunga mkono hatia dhidi ya Trump katika kutumia vibaya madaraka.

Kwa msingi huo, mchakato ambao ulianza kwa kufichuliwa taarifa za siri za mazungumzo yenye utata ya simu baina ya Trump na Rais wa Ukraine umemalizika kwa Baraza la Seneti kumuondoa hatiani Trump.

Pamoja na hayo, haimaanishi kuwa hatua ya Baraza la Seneti kumuondoa hatini ni mwisho wa kashfa ya 'Ukraine-Gate'; hasa kwa kuzingatia kuwa Maseneta wa chama cha Republican, kinyume na ilivyokuwa kesi zingine za kuwauzulu marais, hawakuruhusu mashahidi wapya waitwe katika kikao cha mahakama.

Bunge la Seneti la Marekani likisikiliza kesi ya kumuuzulu Trump

Maudhui hii inapata umuhimu zaidi kwa kuzingatia kuwa inatabiriwa kuwa, John Bolton, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa katika Ikulu ya White House na Mick Mulvaney kaimu mkuu wa Idara ya Wafanyakazi wa Ikulu ya White House wana taarifa kamili katika kuishinikiza Ukraine. Iwapo taarifa hizo zingetolewa zingeweza kubadilisha mchakato wa kesi ya Trump katika Seneti. Lakini kwa kuzingatia kuwa Maseneta wa chama cha Republican ambao walikuwa wanaongoza kesi hiyo walikuwa wameapa kumuunga mkono Trump, hatimaye  Seneti imemuondoa hatiani.

Pamoja na hayo uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, wananchi waliowengi wa Marekani hawajaridhishwa na uamuzi wa Seneti na wanaamini kuwa Trump ana hatia katika kashfa ya Ukraine-Gate.

Kwa ujumla, uchunguzi wa maoni umebaini kuwa, takribani nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa Trump amefanya kosa na alistahili kuuzuliwa kama rais. Pamoja na kuwa nusu ya Wamarekani wana mtazamo hasi kumuhusu Rais Trump, lakini Maseneta wamepiga kura kwa msingi wa chama na hivyo wamemnusuru. Kwa hivyo matumaini ya Wamarekani kumuondoa madarakani Trump sasa yamesalia katika uchaguzi wa rais mwezi Novemba.

Katika historia ya Marekani hii ni mara ya kwanza kwa  kwa rais wa nchi kukabiliwa na kesi ya kuuzuliwa katika kipindi cha kwanza ikiwa imesalia miezi kadhaa kabla ya uchaguzi.

Seneta Chuck Schumer

Wademokrat wana matumaini kuwa, ufichuaji  ambao umejiri katika mchakato wa kumuuzulu Trump umeweka wazi uvunjaji sheria na utumiaji vibaya madaraka wa rais huyo  na hivyo unaweza kuwapelekea kupata ushindi katika uchaguzi wa rais mwaka huu.

Pamoja na hayo, bado haijabainika wazi ni kipi kitakachojiri katika siku ya uchaguzi hasa kwa kuzingatia kuwa Wademocrat bado wako katika mchakato wa kumteua mgombea wao katika uchaguzi wa Novemba. Lakini kile kilicho wazi ni kuwa, kasfa ya Ukraine-Gate haitaishia katika Seneti  bali itabakia kama jeraha la muda mrefu katika siasa za Marekani.

Seneta Chuck Schumer kiongozi wa waliowachache katika Bunge la Seneti amekosoa vikali mchakato wa kumuuzulu Trump na kusema 'huu ni mwanzo wa kumalizika demokrasia." Hakuna shaka kuwa pia huo utakuwa mwanzo wa mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na kisheria Marekani.