Feb 11, 2020 07:59 UTC
  • Iran na Ukraine zasisitizia kutoingizwa siasa katika suala la kuanguka ndege ya Ukraine

Katibu Mkuu wa Baraza la Uslama wa Taifa la Iran na Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ukraine, kwa pamoja wamesisitiza kutoingizwa siasa katika faili la kuanguka ndege ya abiria ya Ukraine nchini hapa.

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Januari mwaka huu, ndege moja ya abiria ya Shirika la Ndege la Ukraine, ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini (MA) mjini Tehran ambapo katika ajali hiyo abiria 167 na wahudumu 9 walipoteza maisha. Katika uwanja huo, Jumatatu ya jana Admeli Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alifanya mazungumzo ya simu na Oleksiy Danilov, Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ukraine ambapo alisema kuwa ni dharura kwa nchi mbili kufanya juhudi za kuzuia kuingizwa utashi wa pande zingine katika suala hilo na hivyo kutumiwa vibaya mwenendo wa uchunguzu wa kifufundi na kiutaalamu wa faili hilo. Aidha Shamkhani amefafanua kuwa, tukio hilo chungu lilitokana na makosa ya kibinaadamu na haifai kuruhusu uingiliaji wa pande zenye chuki na malengo ya kisiasa katika faili hilo. 

Ali Shamkhani, Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran

Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran sambamba na kumwalika Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ukraine kuitembelea Iran kwa lengo la kufuatilia mwenendo wa uchunguzi wa pamoja wa faili hilo unaotekelezwa na asasi za usalama wa taifa za nchi mbili kwa kuhudhuriwa na wataalamu wa kiufundi, amesisitiza kuwa kufikiwa tathmini ya kiufundi kwa makubaliano ya pamoja kunaweza kuainisha hatima ya faili hilo katika anga ya kitaalamu na mbali na wigo wa kisiasa. Naye Oleksiy Danilov, Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ukraine katika mazungumzo hayo ya simu, sambamba na kubainisha kuwa kuharakishwa mwenendo wa kubaini sababu za tukio hilo kunaweza kuzuia uingiliwaji wa pande nyingine za kigeni, amesema kuwa Tehran na Kiev ni lazima ziendeleze ushirikiano na kuharakisha mwenendo wa kutangazwa matokeo ya mwisho ya faili hilo.

Tags