Marekani yafanya mazoezi ya vita vya kinyuklia dhidi Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59326-marekani_yafanya_mazoezi_ya_vita_vya_kinyuklia_dhidi_russia
Jeshi la Marekani limefanya mazoezi ya kuishambulia Russia kwa silaha za nyuklia huku mzozo ukizidi kutokota kati ya madola hayo mawili yenye uwezo mkubwa zaidi wa silaha za nyuklia duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2020 21:46 UTC
  • Marekani yafanya mazoezi ya vita vya kinyuklia dhidi Russia

Jeshi la Marekani limefanya mazoezi ya kuishambulia Russia kwa silaha za nyuklia huku mzozo ukizidi kutokota kati ya madola hayo mawili yenye uwezo mkubwa zaidi wa silaha za nyuklia duniani.

Kwa mujibu wa taarifa mazoezi hayo yalifanywa siku chache zilizopita  katika Kamandi ya Kistratijia ya Jeshi la Marekani jimboni Nebraska na kuhudhuriwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper.

Afisa wa Jeshi la Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema mazoezi hayo yalihusu kinachoweza kujiri iwapo kutaibuka vita vya kinyuklia baina ya Ulaya na Russia na namna ambavyo Marekani, kama mwanachama wa NATO, itaingia katika vita hivyo.

Mapema mwezi huu Marekani ilitangaza kuzindua makombora mapya ya masafa marefu ambayo yatasheheniwa na nyambizi zake ambazo ni ngumu kutambulika zikiwa baharini.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper (aliyevalia tai ya njano) akiwa katika Kamandi ya Kistratijia ya Jeshi la Marekani jimboni Nebraska

Rais Donald Trump wa Marekani anatekeleza mkakati wa kuiondoa nchi yake katika mikataba muhimu ya kimataifa ya kudhibiti silaha za nyuklia ili nchi hiyo iwe na uhuru zaidi wa kuimarisha uwezo wake wa silaha hizo za maangamizi ya umati.

Mpango huo wa Marekani umewaweka wasiwasi mkubwa waitifaki wake barani Ulaya; hasa nchi kama vile Ufaransa ambayo imeanzisha mchakato wa kupunguza silaha zake za nyuklia.