India yatakiwa kuheshimu haki za raia wote wakiwemo Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59638-india_yatakiwa_kuheshimu_haki_za_raia_wote_wakiwemo_waislamu
Kituo cha Mawakili cha Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimelaani vikali mauaji yanayofanywa nchini India dhidi ya Waislamu na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuheshimu misingi na kanuni za haki za raia wote wa nchi hiyo wakiwemo Waislamu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 09, 2020 07:33 UTC
  • India yatakiwa kuheshimu haki za raia wote wakiwemo Waislamu

Kituo cha Mawakili cha Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimelaani vikali mauaji yanayofanywa nchini India dhidi ya Waislamu na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuheshimu misingi na kanuni za haki za raia wote wa nchi hiyo wakiwemo Waislamu.

Taarifa ya Kituo cha Mawakili cha Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyotolewa jana imeitaka serikali ya India ifanye mambo kwa misingi na sheria za haki za binadamu za kimataifa kama kuhakikisha kunakuweko uadilifu na usawa na kulidhamini hilo kwa mila, kaumu na dini zote nchini humo.

Aidha kituo hicho kimezitaka nchi za Kiislamu hususan Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kutekeleza majukumu yake ya kidini na kibinadamu katika kutetea haki za Waislamu wa India.

Mawakili hao wameitaka OIC kutumia uwezo wake wote na kuishinikiza serikali ya India ili ihitimishe vurugu zinazoshuhudiwa hivi sasa dhidi ya Waislamu na kutekeleza siasa za kuishi kwa pamoja na kwa amani baina ya kaumu na dini mbalimbali nchini humo.

Itakumbukwa kuwa Desemba 11, 2019 Bunge la India lilipasisha marekebisho ya sheria ya uraia ambayo yanawapa haki ya uraia wahajiri wasio Waislamu wanaolazimika kuhama nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan na kuhamia India; lakini haki hiyo haitawahusu wahajiri kutoka nchi hizo ambao watakuwa ni Waislamu.

Baada ya Waislamu na wasio Waislamu nchini India kuandamana kupinga sheria hiyo ya kibaguzi, Wahindu wenye misimamo ya chuki na uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu wamewashambulia Waislamu na matukufu yao ikiwemo misikiti kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, New Delhi.