Kujiondoa rasmi Marekani katika Shirika la Afya Duniani WHO
Msimamo wa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani ni kupuuza, kukosoa, kutoa vitisho na hatimaye kujitoa katika mashirika ya kimataifa na hasa yale yanayopinga matakwa na maslahi haramu ya nchi hiyo na ya washirika wake na hasa utawala haramu wa Israel.
Hatua rasmi iliyochukuliwa hivi karibuni na nchi hiyo ni kujitoa katika Shirika la Afya Duniani, WHO. Katika uwanja huo, Seneta Bob Menendez wa chama cha Democrat wa jimbo la New Jersey alisema Jumanne kwamba Rais Trump ameiondoa rasmi Marekani katika shirika hilo. Huku akikosoa namna hatua hiyo ilivyochukuliwa kwa pupa na bila ya tahadhari yoyote, Menendez amesema kuwa kuchukuliwa hatua hiyo isiyo ya busara tena katika mazingira haya ambapo Marekani imepata pigo kubwa kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona kutahatarisha usalama wa mamilioni ya wagonjwa wa Wamarekani ambao tayari wanasumbuliwa na virusi hivyo.
Kusambaa kwa kasi virusi ya COVID-19 nchini Marekani ambayo sasa ndiyo inayoongoza ulimwenguni kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walioambakizwa virusi hivyo, kumepelekea serikali ya Trump kukabiliwa na ukosoaji mkali kutokana na kuzembea katika kuchukua hatua za dharura za kupambana na ugonjwa huo. Ili kukabiliana na ukosoaji huo, Trump amejaribu kutumia kila njia za upotoshaji ikiwemo ya kulilaumu shirika la WHO kuwa ndilo lililosababisha hali hiyo ya kusikitisha ya waathirika wa corona nchini Marekani.
Kwa utaratibu huo, baada ya kushadidi hitilafu na vita vya maneno baina ya serikali yake na shirika la WHO na kudai kuwa shirika hilo linaipendelea China, hatimaye Trump mwezi Aprili mwaka huu alitoa amri ya kukatiwa shirika hilo mchango wa fedha wa Marekani, na hii ni katika hali ambayo shirika hilo linahitajia sana msaada huo kwa ajili ya kupambana na kasi ya kuenea virusi hivyo duniani.
Marekani ambayo imekuwa mchangiaji mkubwa zaidi wa bajeti ya shirika la WHO imedai kuwa itaelekeza mchango huo katika mashirika mengine ambayo yanajishughulisha na masuala ya afya na usalama wa jamii duniani. Hatua hiyo ya Trump imekabiliwa na lawama kali za ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Marekani amesema: Uamuzi wa Trump wa kusimamisha misaada ya kifedha ya Marekani kwa Shirika la Afya Duniani, ni hatari kubwa na usio wa kisheria, ambao tayari umehatarisha usalama na maisha ya Wamarekani pamoja na ya watu wengine duniani.
Nukta muhimu hapa ni kwamba washirika na wapinzani wa Marekani wote kwa pamoja wamechukua msimamo mmoja katika kulaani na kukosoa hatua hiyo isiyo ya busara ya Rais Trump. Wote wanaamini kwamba hatua hiyo katika mazingira hatari ya hivi sasa ya kuenea kwa kasi virusi vya corona duniani, inakwenda kinyume moja kwa moja na ahadi za Marekani za kuyasaidia mashirika ya kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yao na wakati huohuo kutoa pigo kubwa kwa juhudi za jamii ya kimataifa za kukabiliana na ueneaji wa maradhi ya COVID-19.
Jens Spahn, Waziri wa Afya wa Ujerumani pia amekosoa vikali uamuzi wa Marekani wa kukata ushirikiano wake na Shirika la Afya Duniani, na kusema kuwa hatua hiyo inakatisha tamaa na kuwa inarudisha nyumba hatua zote zilizopigwa na WHO katika utekelezaji wa majukumu yake.
Tarehe 29 Mei mwaka huu Trump alidai kwamba shirika la WHO linadhibitiwa na China na kuamua kulikatia misaada yote ya kifedha. Kuondoka rasmi serikali ya Trump katika shirika la WHO kumetathminiwa vibaya na Joe Biden mpinzani wake wa chama cha Democrat katika uchaguzi ujao wa mwezi Novemba. Baada ya serikali ya Trump kutangaza rasmi kujitoa katika WHO Biden aliandika jana Jumatatno kupitia ujumbe mfupi wa Twitter kwa kusema: Wamarekani wako salama zaidi wakati serikali yao inapounga mkono na kuimarisha afya duniani. Nitakapofanikiwa kuingoza Marekani kama rais wa nchi, shughuli yangu ya kwanza ofisini itakuwa ni kuirejesha Marekani katika Shirika la Afya Duniani, na hivyo kurudisha tena uongozi wa Marekani katika ngazi ya kimataifa.
Sisitizo la kurejeshwa Marekani katika shirika hilo la kimataifa linathibitisha wazi kwamba hata wanasiasa wa ngazi za juu wa Marekani pia wanatambua wazi taathira haribifu za siasa za Trump katika mashirika ya kimataifa na pia kile kinachotajwa kuwa ushawishi na ungozi wa nchi hiyo duniani.
Hivi sasa kwa kutangazwa rasmi kujiondoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani WHO, serikali ya Trump imechukua hatua nyingine katika kudhoofisha mashirika ya kimataifa, na hasa kurudisha nyuma juhudi zote za afya ambazo zimefanywa na shirika hilo katika kupambana na Janga la COVID-19.