Guterres atahadharisha kuhusu hatari ya silaha za nyuklia
(last modified Thu, 06 Aug 2020 09:32:28 GMT )
Aug 06, 2020 09:32 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa hatari ya silaha za nyuklia inaongezeka siku baada ya nyingine.

Antonio Guterres ametoa tahadhari hiyo katika ujumbe wake uliotolewa kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 75 tangu baada ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Marekani dhidi ya mji wa Hiroshima nchini Japan tarehe 6 Agosti mwaka 1945 na amezitaka nchi zote kuendelea kuheshimu ahadi zao za kukabiliana na silaha hatari za nyuklia na kufanya jitihada za kusafisha kabisa silaha hizo kote duniani.

Guterres amesema katika ujumbe wa video ulioonyeshwa kwenye kumbukumbu ya shambulizi la bomu la nyuklia la Hiroshima huko magharibi mwa Japan kwamba: Silaha za nyuklia yumkini zikatumiwa kwa makusudi au kimakosa na bila ya kukusudia, na ni vigumu sana kuweza kukabiliana na tishio kama hili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema nchi zote duniani zinaweza kuwa na mchango katika kuangamiza silaha za nyuklia japokuwa nchi zinazomiliki silaha hizo zina majukumu makhsusi katika uwanja huo. 

Wajapani wawakumbuka maelfu ya raia wa nchi hiyo waliouawa na mabomu ya nyuklia ya Marekani.

Tarehe 6 Agosti 1945, ndege moja ya kivita ya jeshi la Marekani aina ya B-29 ilidondosha bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima nchini Japan kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Harry Truman.

Siku tatu baadaye, Marekani iliwadondoshea bomu jengine la atomiki raia wa Japan wa mji wa Nagasaki.

Watu wapatao 220,000 walipoteza maisha kutokana na mashambulio hayo mawili yaliyofanywa na Marekani.