Russia yasisitiza udharura wa kuepusha vita vya silaha za nyuklia
(last modified Fri, 07 Aug 2020 06:22:45 GMT )
Aug 07, 2020 06:22 UTC
  • Sergey Lavrov
    Sergey Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amekosoa siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi hususan Marekani katika suala la kudhibiti silaha za nyuklia na kusema kuwa, kuna ulazima wa kufanyika juhudi za kuzuia uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia.

Sergey Lavrov alisema katika ujumbe wake wa jana kwa washiriki katika kumbukumbu ya mwaka 75 baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya mji wa Hiroshima kwa bomu la nyuklia kwamba: Tarehe 6 Agosti Marekani iliushambulia mji wa Hiroshima kwa bomu la nyuklia na siku tatu baadaye ikaushambulia kwa mabomu hayo mji wa Nagasaki; walimwengu bado wanawakumbuka wahanga wa maafa hayo kwa machungu makubwa. 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa, hii leo hata baada ya kutambua kikamilifu sababu za Vita vya Pili vya Dunia ni vigumu sana kuweza kueleza sababu zilizotolewa na watu waliofanya kitendo hicho cha kinyama. 

Lavrov amesisitiza udharura wa kujiepusha na msuguano wa aina yoyote wa kijeshi baina ya madola yanayomiliki silaha za nyuklia na kusema kuwa Moscow inapendekeza kwa nchi zote kuheshimu suala hilo.

Tarehe 6 Agosti 1945, ndege ya kivita ya jeshi la Marekani aina ya B-29 ilidondosha bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima nchini Japan kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Harry Truman.

Mashambulizi ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki ni fedha ya kihistoria kwa Marekani.

Siku tatu baadaye, Marekani iliwadondoshea bomu jengine la atomiki raia wa Japan wa mji wa Nagasaki. Watu wapatao 220,000 walipoteza maisha kutokana na mashambulio hayo mawili yaliyofanywa na Marekani na maelfu ya wengine walijeruhiwa.