Ufaransa yakaribisha mapatano kati ya Iran na wakala wa IAEA
Ufaransa imekaribisha uamuzi wa Iran wa kuuruhusu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kukagua maeneo mawili ya miradi yake ya nyuklia na kusema hiyo ni hatua kuelekea upande sahihi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imekaribisha makubaliano ya Iran na Wakala wa IAEA na kupongeza kuhusu hatua zisizoegemea upande wowote na za kitaalmu za wakala huo. Aidha imesema kuwa ahadi hiyo ya Iran ni sehemu ya utekelezaji wa mapatano yaliyokamilishwa kati ya nchi hiyo na IAEA.
Kabla ya hapo, China pia iliunga mkono na kukaribisha mapatano hayo na kusema kuwa ina matarajio kuhusu ushirikiano wa pande mbili hizo katika kutekeleza mapatano hayo kwa mafanikio.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zilitoa taarifa ya pamoja mwishoni mwa safari ya Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa IAEA hapa Tehran na baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran kwamba pande mbili zimekubaliana kutatua kwa nia njema masuala yaliyoainishwa na wakala huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo; Iran itatoa fursa kwa hiari kukaguliwa maeneo hayo mawili yaliyoainishwa na wakala wa IAEA na itarahisisha shughuli za ukaguzi wa wakala huo ili kuyapatia ufumbuzi masuala hayo. Pande mbili za Iran na IAEA zimekubalina pia kuhusu tarehe ambayo wakala huo utapaswa kufika katika maeneo hayo yaliyoainishwa na kufanya ukaguzi wake.