Guterres ataka kufungwa vituo vya kuwashikilia wakimbizi nchini Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa Libya kuvifunga vituo vyote ambavyo wakimbizi wamekuwa wakishikiliwa nchini humo.
Antonio Guterres amewasilisha ripoti kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akilalamikia ukiukaji wa haki za wakimbizi unaofanywa katika vituo hivyo vya kuwashikilia watu huko Libya.
Katika ripoti yake hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa hali ya kutisha ya vituo hivyo ambapo wakimbizi huwekwa mahabusu ikiwemo ukosefu wa chakula na huduma za afya pamoja na vitendo vya mabavu na udhalilishaji vinavyofanywa na wafanyakazi wa vituo hivyo yakiwemo mateso na kueleza kuwa: hakuna kitu kinachoweza kuhalalalisha hali ya kutisha waliyo nayo wakimbizi na wahamiaji huko Libya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa; zaidi ya watu 2,780 wamewekwa mahabusu katika vituo vya kuwashikilia wahamiaji haramu katika kona mbalimbali za Libya.