Lavrov apinga tuhuma kwamba Russia inaingilia uchaguzi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63390-lavrov_apinga_tuhuma_kwamba_russia_inaingilia_uchaguzi_wa_marekani
Uhusiano wa Russia na Marekani umekuwa na mivutano mikubwa baada ya kutokea mgogoro huko Ukraine mwaka 2014. Moja ya kadhia ambazo zimebadilika huko Marekani katika miaka ya karibuni na kuwa dhidi ya Moscow ni mjadala wa madai ya Russia kuingilia uchaguzi wa Marekani. Kwa kuzingatia kukaribia kufanyika uchaguzi wa Rais wa Marekani hivi sasa soko la tuhuma hizo limezidi kupamba moto.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2020 03:04 UTC
  • Lavrov apinga tuhuma kwamba Russia inaingilia uchaguzi wa Marekani

Uhusiano wa Russia na Marekani umekuwa na mivutano mikubwa baada ya kutokea mgogoro huko Ukraine mwaka 2014. Moja ya kadhia ambazo zimebadilika huko Marekani katika miaka ya karibuni na kuwa dhidi ya Moscow ni mjadala wa madai ya Russia kuingilia uchaguzi wa Marekani. Kwa kuzingatia kukaribia kufanyika uchaguzi wa Rais wa Marekani hivi sasa soko la tuhuma hizo limezidi kupamba moto.

Tuhuma hizo zimekumbwa na radiamali ya Russia. Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia juzi Ijumaa alizitaja tuhuma zilizoelekezwa kwa nchi yake kwamba inatumia wadukuzi kwa lengo la kuingilia masuala ya ndani ya Marekani kuwa hazina msingi wowote. Hivi karibuni kampuni ya Microsoft ilidai kuwa wadukuzi wenye mfungamano na Russia wamefanya jitihada za kuwajasusi watu wa karibu na Donald Trump na Joe Biden wagombea wa kiti cha urais nchini Marekani wa vyama vya Democrats na Republican. 

Lavrov amebainisha kuwa, ni Marekani yenyewe ndiyo inayotumia njia zilizo kinyume cha sheria kwa maslahi yake. Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia amesema katika mkutano na waandishi habari kuwa: Russia haijawahi kuingilia uchaguzi wa Marekani na haina mpango wa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo au nchi nyingine yoyote. 

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia  

Wizara ya Fedha ya Marekani siku chache zilizopita ilitangaza habari ya kujumuishwa majina ya raia wanne wa Russia katika faharasa ya vikwazo ya Ofisi ya Kudhibiti Fedha za Kigeni ambayo ni moja ya taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo. Taarifa hiyo ilidai kuwa raia wanne wa Russia walifanya kila wawezalo kuathiri mchakato wa uchaguzi wa rais nchini Marekani na kudhofisha taasisi za kidemokrasia nchini humo. Pamoja na hayo, hakuna ushahidi wowote wenye mashiko uliotolewa hadi sasa wa kuthibitisha tuhuma hizo za uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa Marekani. 

Naye William Evanina, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kupaambana na Ujasusi na Kulinda Usalama wa Marekani mwezi Agosti mwaka huu alidai kuwa Russia, China na Iran zinafanya operesheni za siri na za wazi wazi ili kuathiri uchaguzi wa mwaka huu huko Marekani. Alisema kuwa, serikali za nchi hizo zinataka kushinda mgombea zinayemtaka. 

Moscow kwa upande wake inaona kuwa, ni Marekani yenyewe ndiyo ambayo siku zote inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyinginezo kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja na imekuwa ikifanya juu chini ili kubadili michakato mbalimbali ya kisiasa kwa maslahi yake. Russia imeshuhudia mara kadhaa Marekani ikiingilia waziwazi uchaguzi wake na pia kuwachochea wapinzani wa serikali ya Russia kuandamana kupinga matokeo ya chaguzi za bunge au rais za Russia. 

Ukweli ni kuwa, chuki dhidi ya Russia imeipelekea Marekani kuanzisha vita vya moja kwa moja vya kipropaganda na vya vyombo vya habari katika chaguzi kadhaa za karibuni za Russia dhidi ya serikali ya Moscow na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.  Katika upande mwingine, tangu kufanyika uchaguzi wa rais nchini Marekani mwaka 2016 na baada ya Trump kutangazwa mshindi katika uchaguzi huo, viongozi wa Marekani wamekuwa wakizusha makelele mengi kwamba Russia iliingilia uchaguzi huo wa rais kwa maslahi ya Trump na kwa madhara ya Hillary Clinton mgombea wa chama cha Democrat; na hata serikali ya Obama mwezi Disemba mwaka 2016 ilichukua hatua na kuamua kufunga baadhi ya ofisi za kidiplomasia za Russia huko Marekani na kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo kwa kisingizio hicho. Hivi sasa pia Wademocrat wanasema wana wasiwasi kama huo. 

Kamala Harris, mgombea mwenza wa Joe Biden katika uchaguzi ujao wa Rais wa Marekani tarehe 6 mwezi huu alieleza kuwa:"  kama Biden atashindwa katika uchaguzi huo hiyo itakuwa ni kutokana na uingiliaji wa Russia." Huko nyuma pia viongozi wengine rasmi wa Marekani kama Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alidai kwamba, Russia, Iran na China zina lengo la kuingilia uchaguzi wa rais huko Marekani.  

Harrisa Kamala, mgombea wa kiti cha Makamu wa Rais kwa tiketi ya chama cha Democrat nchini Marekani  

Madai haya yametolewa hivi sasa na Wademocrat ili kutokubali matokeo ya uchaguzi iwapo watashindwa kwenye uchaguzi. Pavel Sharikov mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Russia anasema: Sababu ya kuingia dosari uhusiano wa Marekani na Russia ni kwamba, kadhia ya Russia imegeuzwa kuwa ushindani wa kisiasa wa ndani ya Marekani."