UN: Mazungumzo ya amani Libya yamalizika; Imarati bado yatuma silaha kimagendo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63743-un_mazungumzo_ya_amani_libya_yamalizika_imarati_bado_yatuma_silaha_kimagendo
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mazungumzo ya makundi mbalimbali ya Libya ya kutafuta amani ya nchi yao yamemalizika nchini Misri na matokeo ya mazungumzo hayo ni mazuri.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 01, 2020 02:31 UTC
  • UN: Mazungumzo ya amani Libya yamalizika; Imarati bado yatuma silaha kimagendo

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mazungumzo ya makundi mbalimbali ya Libya ya kutafuta amani ya nchi yao yamemalizika nchini Misri na matokeo ya mazungumzo hayo ni mazuri.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, vikao viwili vya makamanda wa kijeshi wa kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" na wale wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya nchi hiyo vilivyofanyika nchini Misri, vimezeaa matunda mazuri.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulioshiriki kwenye mazungumzo hayo umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, moyo ya kuhisi wajibu wa kubeba majukumu, uwazi na kuaminiana ndivyo vitu vilivyotawala vikao hivyo.

Mwishoni mwa mazungumzo hayo, pande zote zimetilia mkazo mambo mbalimbali ukiwemo wajibu wa kufanyika haraka vikao vya kamati ya pamoja ya kijeshi ijulikanayo kwa jina la 5+5, kukomeshwa mashambulizi ya maneno baina ya pande mbili na kuharakishwa njia za usafiri na uchukuzi wa angani na ardhini ili kuruhusu raia wote wa Libya wanafanya safari zao kwa uhuru na usalama.

Nchi kama Imarati ni wachochezi wakubwa wa mapigano nchini Libya

 

Hata hivyo na licha ya kupatikana mafanikio hayo, lakini kuna baadhi ya nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinaonesha hazipendi kuona amani inapatikana nchini Libya.

Hii ni kwa sababu, mwanadiplomasia mmoja Mmarekani katika Umoja wa Mataifa amefichua yaliyomo kwenye ripoti moja ya siri inayoonesha kuwa Imarati haiheshimu vikwazo vya silaha na vya anga ilivyowekewa Libya.

Mwanadiplomasia huyo amenukuliwa na Shirika la Habari la FARS akifichua kuwa, Imarati inaendelea kuwatumia silaha kimagendo wanamgambo inaowaunga mkono wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" licha ya Umoja wa Mataifa kupiga marufuku jambo hilo.