COVID-19 Ulaya: Sheria za udhibiti zaibua ghasia Uhispania, Uingereza yafungwa
Bara Ulaya sasa linakabiliana na wimbi la pili la maambukizi ya COVID-19 au corona huku hali ikitabiriwa kuendelea kuwa mbaya katika wiki kadhaa zijazo.
Nchini Uhispania wananchi wamenadamana katika miji mbalimbali baada ya serikali kutangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi sita ili kukabiliana na janga la corona. Sheria hiyo ya hali ya hatari inawapa maafisa wa serikali za kieneo uwezo wa kutekeleza sheria za kutotoka nje na kuzuia safari ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez amelaani machafuko yaliyosababishwa na maandamano hayo na kusema serikali yake haitastahamili maandamano ya wanaoibua ghasia. Hadi sasa watu 35,878 wamepoteza maisha kutokana na corona nchini Uhispania. Sheria kali za kuzuia maambukizi ya corona pia zimeanza kutekelezwa upya Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji, Austria na Uingereza.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema nchi hiyo itaweka vikwazo vikali kwa wakazi wake wiki ijayo kama sehemu ya kuzuia ongezeko la maambukizi yanayoongezeka ya virusi vya corona. Haya yanajiri wakati ambapo Uingereza imefikia maambukizi milioni moja ya virusi hivyo hapo jana. Maduka yasiyouza bidhaa za lazima pamoja na maeneo ya starehe yatafungwa kuanzia Alhamis hadi Disemba 2.
Kwa mujibu wa jarida la Wall Street Journal, kwa wastani watu 1,370 wanapoteza maisha kila siku katika nchi za Umoja wa Ulaya na Uingereza kutokana na corona. Ripoti hiyo imeongeza kuwa nchini Marekani, kwa wastani watu 808 wanapoteza maisha kila siku kutokana na corona.