Putin akosoa dini kuvunjiwa heshima kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64469-putin_akosoa_dini_kuvunjiwa_heshima_kwa_kisingizio_cha_uhuru_wa_kujieleza
Kuongezeka vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu (saw) nchini Ufaransa na kuungwa mkono vitendo hivyo na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema na kujieleza, ni jambo ambalo limeamsha hasira kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 07, 2020 02:29 UTC
  •  Vladimr Putin
    Vladimr Putin

Kuongezeka vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu (saw) nchini Ufaransa na kuungwa mkono vitendo hivyo na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema na kujieleza, ni jambo ambalo limeamsha hasira kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu.

Mara hii Rais Vladimr Putin wa Russia kwa upande wake amechukua msimamo dhidi ya tabia hiyo ya nchi za Magharibi kuvunjia heshima matukufu ya kidini. Akizungumza hivi karibuni katika kikao na viongozi wa dini tofauti za Russia na kwa kuzingatia kukasirishwa Waislamu ulimwenguni na msimamo wa kibaguzi wa hivi karibuni wa serikali ya Ufaransa dhidi ya Waislamu, Rais Putin amesisitiza kuwa uhuru wa kujieleza haupasi kutumika kuwaudhi wafuasi wa dini nyingine. Ametaka hatua za dharura zichukuliwe kwa ajili ya kuzuia hitilafu za kidini.

Msimamo huo wa Putin kwa hakika ni ukosoaji wake dhidi ya msimamo wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye ametetea kwa nguvu zake zote kitendo cha jarida moja la nchi hiyo cha kuchapisha vikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw), kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema katika nchi hiyo ya Ulaya. Msimamo huo wa kibaguzi na wa kupindukia wa Macron na serikali yake umeibua hisia kali katika pembe tofauti za dunia na hasa katika ulimwemgu wa Kiislamu ambapo katika siku za karibuni kumetokea mashambulizi ya silaha baridi na moto nchini Ufaransa kwenyewe na vilevile Austria. Putin amekemea misimamo ya kupindukia mpaka katika pande zote mbili kwa kusema, tunashuhudia vitendo vya chuki vikitekelezwa na baadhi ya watu wanaotumia kisingizio cha uhuru wa kujieleza kuwaudhi wafuasi wa dini nyingine, na wakati huohuo watu waliochukizwa na jambo hilo kuchukua misimamo ya kupindukia mpaka kwa kuhalalisha vitendo vyao vya mabavu na kutovumilia wenzao.

Macron aliye na chuki kali dhidi ya Uislamu

Msimamo wa Putin akiwa kiongozi wa nchi ya Kikristo inayofuata madhehebu ya Orthodox, unathibitisha wazi kwamba hakubaliani na msimamo na siasa za nchi za Magharibi zinazodai kuwa ni za Kikristo na ambazo zinaendesha siasa za chuki na uhasama dhidi ya Uislamu. Anaamini kuwa msimamo wa nchi hizo za Magharibi si msimamo wa mafundisho ya Kikristo. Wakati huo huo, matukio ya umwagaji damu ya hivi karibuni huko Ufaransa na Austria na msimamo mkali wa Macron wa kuendelea kuunga mkono vikatuni vinavyochapishwa na jarida la Charlie Hebdo kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kujieleza, bila shaka ni mwenendo hatari ambao hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha mvutano na ghasia katika jamii ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa Sayyid Hadi Burhani, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi, Ufaransa ni moja ya nchi za Ulaya ambazo zinaruhusu na kuchochea zaidi vitendo vya kutusiwa thamani na matukufu ya kidini. Hii ni pamoja na kuwa kisingizio kinachotumiwa na Macron kuwaruhusu wenye chuki dhidi ya Uislamu kuvunjia heshima matukufu ya dini ni jambo linaenda kinyume na baadhi ya sheria za Ufaransa. Taarifa iliyotolewa Jumatano na wasomi wa Kiislamu ikiwahutubu watu wote duniani na hasa Wafaransa, imesisitiza kwamba demokrasia ya kindumakuwili inayotumika kuibagua jamii moja na kuipendelea nyingine sio demokrasia ya kweli.

Matakwa ya kususiwa bidhaa za Ufaransa kufuatia chuki ya Macron dhidi ya Uislamu na Mtume Mtukufu (saw)

Taarifa hiyo imesema kwamba Ufaransa ina sheria za kutetea haki za binadamu zikiwemo za kukabiliana na ubaguzi wa rangi, chuki na ubaguzi ambao unapasa kuwa msingi mzuri wa kulaaniwa na kukemea uvunjiwahi heshima matukufu ya kidini. Sheria hizo zinasema kuwa ni hatia kubagua au kuvunjia heshima dini na hata kuainisha adhabu inayopasa kutolewa kuhusu hatia hiyo. Sheria hizo zinawakataza raia wa Ufaransa kutusi na kuwachukia wenzao kwa misingi ya dini, kabila, taifa na rangi na mambo mengine yanayozua tofauti kati yao.

Vilevile sheria nyingine iliyopitishwa tarehe 13 Mei mwaka huu nchini Ufaransa inapiga marufuku chuki zinazoenezwa kupitia mtandano wa interneti. Kwa msingi huo ni wazi kuwa kutumika kisingizio cha uhuru wa kujieleza kwa ajili ya kuutusi Uislamu na Mtume wake Mtukufu (saw) ni jambo linalotekelezwa tu kutokana na chuki waliyonayo Wamagharibi dhidi ya Uislamu.