Vijana Waislamu wa Ufaransa wajitolea kulinda makanisa ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64491-vijana_waislamu_wa_ufaransa_wajitolea_kulinda_makanisa_ya_nchi_hiyo
Licha ya hatua na matamshi ya kiuadui na ya chuki yaliyotolewa na viongozi wa Ufaransa dhidi ya Uislamu, kundi moja la vijana Waislamu Wafaransa wamejitolea kulinda usalama wa makanisa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2020 23:07 UTC
  • Vijana Waislamu wa Ufaransa wajitolea kulinda makanisa ya nchi hiyo

Licha ya hatua na matamshi ya kiuadui na ya chuki yaliyotolewa na viongozi wa Ufaransa dhidi ya Uislamu, kundi moja la vijana Waislamu Wafaransa wamejitolea kulinda usalama wa makanisa ya nchi hiyo.

Televisheni ya ABC News imeripoti kuwa, kundi moja kutoka jamii ya Waislamu wa Ufaransa hususan vijana wamejitolea kulinda makanisa na hujuma na mashambulio ya kigaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya shambulio la kigaidi lililotokea Alkhamisi ya tarehe 29 Oktoba ndani ya kanisa la Notre Dame katika mji wa Nice mashariki mwa Ufaransa na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watatu, katika hatua ya kuonyesha mshikamano na Wakristo wa nchi hiyo, kundi moja la vijana Waislamu wamekuwa wakijumuika pamoja katika siku za mwisho wa wiki kulinda kanisa kuu la mji wa Lodève kusini mwa nchi hiyo.

Hatua hiyo ya vijana hao wa Kiislamu imewaathiri mno viongozi wa wa kanisa hilo ambao wameielezea kuwa ni hatua yenye kutia matumaini makubwa.

Ripoti ya ABC News imeongeza kuwa, kwa mtazamo wa jamii ya Waislamu wa Ufaransa shambulio la karibuni liliofanywa na mtu mmoja kwa kutumia silaha baridi ndani ya kanisa la Notre Dame huko mjini Nice halina uhusiano wowote na Uislamu.

Itakumbukwa kuwa baada ya kuuawa mwalimu mmoja wa Kifaransa aliyeonyesha darasani picha za vikatuni vya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW, rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron aliunga mkono kuendelea kuchapishwa vikatuni hivyo kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni.

Matamshi hayo machafu ya Macron yalichochea mashambulio kadhaa ya kigaidi ndani ya Ufaransa.

Lakini mbali na nchini humo, msimamo huo wa kiongozi huyo umelaaniwa vikali na Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia.

Mbali na maandamano makubwa yaliyofanyika katika nchi mbalimbali kulaani msimamo wa Macron dhidi ya Uislamu zinaendeshwa kampeni pia za kususia bidhaa za Ufaransa.../