Dec 03, 2020 07:24 UTC
  • Takwimu rasmi: Wajapan wanaojiua ni wengi zaidi kuliko wanaofariki kwa corona!

Takiwmu zilizotolewa na serikali ya Japan zinaonyesha kuwa, katika mwezi wa Oktoba pekee, watu 2,215 walijiua nchini humo, idadi ambayo ni kubwa zaidi kulinganisha na ya watu wote walioaga dunia hadi sasa nchini humo kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Takwimu rasmi za Shirika la Taifa la Polisi ya Japan zinaonyesha kuwa watu 2,215 walijiua katika mwezi wa Oktoba, wakati idadi ya watu wote walioaga dunia kwa virusi vya corona nchini humo hadi sasa ni 2,172!

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa muda mrefu Japan imekuwa miongoni mwa nchi duniani ambazo zina kiwango cha juu cha watu wanaojiua, ambapo katika mwaka 2016 kati ya kila watu laki moja nchini humo, 18 miongoni mwao walijinyonga kikiwa ni kiwango cha juu zaidi katika eneo la Bahari ya Mediterania Magharibi baada ya Korea Kusini, na takriban mara mbili zaidi ya wastani wa dunia nzima kwa mwaka, ambao ni watu wapatao 10 kati ya kila watu laki moja.

Japan ni katika nchi zenye kiwango cha chini cha idadi ya watu wanaofariki kwa Covid-19

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Japan, katika kipindi cha miaka 10 iliyoishia mwaka 2019, idadi ya watu waliofariki kwa kujiua nchini humo ilikuwa imepungua, ambapo katika mwaka uliopita wa 2019 idadi hiyo ilipungua hadi  watu elfu 20, lakini idadi hiyo imeongezeka katika mwaka huu wa 2020 sambamba na kuzuka janga la dunia nzima la maambukizi ya virusi vya corona.

Ripoti ya wizara hiyo imeeleza kuwa, muda mwingi wa saa za kazi, kutengwa kijamii na mashinikizo ya kimawazo ni miongoni mwa sababu kuu za watu kujiua nchini Japan.../

Tags