Kupaswisha azimio dhidi ya Iran katika Bunge la Ulaya
Wabunge wa Umoja wa Ulaya jana Alkhamisi walipasisha azimio linaloituhumu Iran kuwa inakiuka haki za binadamu
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, azimio hilo lilipasishwa kwa kura 614 za ndio, 12 za hapana na wabunge wengine 63 wakajizuia kupiga kura kwa maslahi ya upande wowote, na hivyo kupitishwa azimio hilo linaloikosoa Iran kwa kumnyonga Ruhollah Zam.
Awali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imekosoa hatua na taarifa za nchi za Magharibi kuhusiana na adhabu ya kifo iliyotolewa kwa kibaraka wao huyo aliyehusika na uchochezi wa ghasia na machafuko nchini Iran kwa maslahi ya nchi hizo na kusisitiza kuwa Iran inaheshimu misingi yote ya sheria za kimataifa zikiwemo za kulinda haki za binadamu.
Pamoja na hayo Tehran imesema kuwa haitakubali nchi za kigeni kuingilia mambo yake ya ndani kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kijieleza na haki za binadamu. Imelaani vikali uchochezi wa kisiasa na kiusalama unaofanywa na nchi hizo dhidi ya usalama wa taifa la Iran.
Wabunge wa Umoja wa Ulaya wameingilia moja kwa moja mambo ya ndani ya Iran kwa kukosoa uamuzi uliotolewa na mahakama za Iran dhidi ya kibaraka Ruhollah Zam aliyehusika na vitendo vingi vinavyohatarisha usalama wa Iran kwa maslahi ya nchi za Magharibi, katika hali ambayo nchi hizo hizo huwa hazichukue hatua yoyote ya kulaani au kukosoa ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa na nchi waitifaki na washirika wao katika eneo.
Ruhollah Zam, aliyekuwa mmoja wa vinara wa kuendesha propaganda na vita vya kisaikoilojia dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran alinyongwa Jumamosi iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi dhidi ya Iran, kuvujisha habari zinazohusiana na harakati za makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Iran, na hasa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kushirikiana na Marekani katika kushadidisha vikwazo vya kidhulma dhidi ya raia wa Iran na kutoa mafunzo ya namna ya kufanya uasi na machafuko dhidi ya mfumo wa Kiislamu nchini.