Mwanasiasa wa Ufaransa ataka marufuku ya hijabu katika maeneo ya umma
https://parstoday.ir/sw/news/world-i66268-mwanasiasa_wa_ufaransa_ataka_marufuku_ya_hijabu_katika_maeneo_ya_umma
Mwanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kulia na mwenye misimamo mikali wa Ufaransa ametoa pendekezo la kupigwa marufuku uvaaji wa vazi la stara la hijabu katika maeneo yote ya umma nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2021 04:49 UTC
  • Mwanasiasa wa Ufaransa ataka marufuku ya hijabu katika maeneo ya umma

Mwanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kulia na mwenye misimamo mikali wa Ufaransa ametoa pendekezo la kupigwa marufuku uvaaji wa vazi la stara la hijabu katika maeneo yote ya umma nchini humo.

Marine Le Pen ambaye alimbwagwa na Rais Emmanuel Macron katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 alitoa mwito huo jana Ijumaa na kudai kuwa, mitandio inayovalia kichwani ni vazi la Kiislamu na kwa msingi huo vazi hilo linapaswa kupigwa marufuku katika maeneo yote ya umma nchini Ufaransa.

Wadadisi wa mambo wanasema mwanasiasa huyo ameanza tena kutumia matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, kama sehemu ya kampeni zake za mapema, kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao 2022.

Wiki mbili zilizopita, Waziri mshauri wa masuala ya uraia wa Ufaransa alitoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu kwa kutaka uvaaji wa vazi la stara la Kiislamu la hijabu nchini humo uwekewe mipaka zaidi.

 

Mwanasiasa mwenye chuki dhidi ya Uislamu, Marine Le Pen

Marlène Schiappa, alitoa matamshi hayo ya chuki dhidi ya Uislamu na kuongezea kusema kwamba, hawezi kuvumilia kuona watoto wadogo wanavaa hijabu. Schiappa amependekeza viongezwe vifungu vingine katika sheria inayopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.

Wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na kampeni za kuichafua dini hii tukufu limeongezeka mno nchini Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni, katika hali ambayo nchi hiyo ndiyo yenye Waislamu wengi zaidi barani Ulaya. Oktoba mwaka jana, Baraza la Seneti la Ufaransa lilipasisha muswada wa sheria inayowapiga marufuku akina mama wanaovaa hijabu kuandamana na watoto wao katika safari za kishule.