Hatua mpya ya Ufaransa ya kuwabana Waislamu wasivae Hijabu yalaaniwa vikali
Uamuzi wa Baraza la Seneti la Ufaransa wa kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma umelaaniwa na kukosolewa vikali ndani ya nchi hiyo na katika kila pembe ya dunia.
Wanaharakati katika mitandao ya kijamii nchini Ufaransa na katika pembe mbali mbali za dunia wameanzisha kampeni kwa anuani ya #"Usiguse Hijabu Yangu" kulaani hatua ya Seneti ya nchi hiyo ya kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa hijabu katika maeneo ya umma.
Mbali na nchini Ufaransa, wanaharakati wa mitandao ya kijamii katika nchi zingine duniani, nao pia wamekosoa vikali hatua ya serikali ya Rais Emmanuel Macron ya kuzidi kuwawekea mbinyo Waislamu wa nchi hiyo kuhusiana na uhuru wa kuabudu.
Kwa mujibu wa mpango huo uliopitishwa na Seneti ya Ufaransa na ambao kama utapitishwa na bunge la taifa utakuwa sheria rasmi, mbali na wasichana wenye umri chini ya miaka 18, akina mama pia watapigwa marufuku kuvaa hijabu watakapokuwa wakiwachukua watoto wao wadogo kuwapeleka skuli.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mswada uliowasilishwa na serikali ya Macron kwa anuani ya "kupiga vita utengano" (anti-separatism).
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, likiwemo la Amnesty International yamekosoa vikali mswada huo yakisisitiza kuwa unalenga kuihujumu na kuibagua jamii ya wachache ya Waislamu wa nchi hiyo.
Mswada huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya uendelezaji wa kampeni ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) barani Ulaya.
Ufaransa yenye Waislamu wapatao milioni tano na laki saba, ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya.../