Taliban wataalikwa katika mazungumzo ya kimataifa ya Moscow kuhusu Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75518-taliban_wataalikwa_katika_mazungumzo_ya_kimataifa_ya_moscow_kuhusu_afghanistan
Russia imesema, italialika kundi la Taliban katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu Afghanistan yaliyopangwa kufanyika tarehe 20 ya mwezi huu wa Oktoba mjini Moscow.
(last modified 2026-02-16T16:36:20+00:00 )
Oct 08, 2021 08:01 UTC
  • Taliban wataalikwa katika mazungumzo ya kimataifa ya Moscow kuhusu Afghanistan

Russia imesema, italialika kundi la Taliban katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu Afghanistan yaliyopangwa kufanyika tarehe 20 ya mwezi huu wa Oktoba mjini Moscow.

Mjumbe maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan Zamir Kabulov ameeleza hayo alipoulizwa na waandishi wa habari wa Russia kama wawakilishi wa Taliban wataalikwa katika mkutano huo utakaozishirikisha pia China, Iran, India na Pakistan.

Mkutano huo wa Moscow utafanyika baada ya kikao cha kundi la G20 kuhusu Afghanistan ambacho kimepangwa kufanyika tarehe 12 Oktoba, ili kuzungumzia jinsi ya kuisaidia nchi hiyo iepukane na maafa ya kibinaadamu kufuatia kundi la Taliban kushika hatamu za uongozi wa nchi.

Kuhusu kama Russia itatoa misaada pia ya kibinadamu kwa Afghanistan, Kabulov amesema, ndiyo itafanya hivyo, lakini suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na shehena ya msaada huo inaendelea kukusanywa.

Kinyume na nchi za Magharibi ambazo zimewaondoa wanadiplomasia wao nchini Afghanistan baada ya Taliban kutwaa madaraka, ubalozi wa Russia katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul unaendelea kufanya kazi.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia amekosoa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Afghanistan na kusema kwamba, Moscow "ilipata somo" kutokana na uvamizi wa Muungano wa Kisovieti katika nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, katika muongo wa 1980, Shirikisho la Urusi ya zamani lilipigana vita vya muongo mzima nchini Afghanistan vilivyosababisha majanga makubwa ya kuuawa Waafghani wapatao milioni mbili mbali na wengine milioni saba waliolazimika kuhama makazi yao sambamba na askari zaidi 14,000 wa Urusi waliouliwa katika vita hivyo.../