Ahadi ya Marekani ya kuilinda Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i78794-ahadi_ya_marekani_ya_kuilinda_ukraine
Jumapili iliyopita Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelinsky, na kujadili jinsi Marekani na washirika wake watakavyojibu shambulio lolote la kijeshi la Russia dhidi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2022 23:15 UTC
  • Ahadi ya Marekani ya kuilinda Ukraine

Jumapili iliyopita Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelinsky, na kujadili jinsi Marekani na washirika wake watakavyojibu shambulio lolote la kijeshi la Russia dhidi ya nchi hiyo.

Taarifa ya Ikulu ya White House imesema, viongozi hao wawili wanaunga mkono suluhisho la kidiplomasia na wanakusudia kufanya jitihada za kuimarisha utulivu wa kistratijia kupitia mazungumzo ya pande mbili kupitia Baraza la NATO-Russia na Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Biden amesisitiza "dhamira ya Marekani" ya kulinda mamlaka ya Ukraine na ardhi ya nchi hiyo, na azma ya Washington na washirika wake ya kumpa Rais wa Ukraine taarifa kamili kuhusu mazungumzo yoyote na Russia. Washington imedai kuwa, Moscow imetuma makumi ya maelfu ya wanajeshi katika mpaka wa Ukraine na Russia kwa shabaha ya kuishambulia nchi hiyo.

Katika mazungumzo yake ya Alkhamisi iliyopita na Rais Putin, Joe Biden alitishia kuiwekea Russia vikwazo vikubwa vya kiuchumi iwapo itaishambulia Ukraine. Licha ya madai ya Marekani na washirika wake wa Ulaya kuhusu eti nia ya Russia kuishambulia Ukraine, ambayo pia yamekaririwa na Rais Zelensky, lakini maafisa wakuu wa usalama wa Ukraine wana maoni tofauti.

Katibu wa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa la Ukraine Oleksiy Miacheslavovych Danilov alisema Jumapili iliyopta kwamba: "Hakuna ushahidi wowote kwamba Rusia ina nia ya kuishambulia Ukraine." Danilov alisema: "Hii leo hatuoni hatari yoyote kutokana na yanayotokea kwenye mipaka yetu. Ikiwa wanamaanisha mkusanyiko mkubwa wa vikosi vya Russia ambavyo vyombo vya habari vya kigeni vinapigia makelele, ninapaswa kusema kwamba hatujaona kitu kama hicho  kabisa."

Oleksiy Miacheslavovych Danilov 

Baraza la Kitaifa la Ulinzi na Usalama la Ukraine linakadiria kuwa takriban wanajeshi 122,000 wa Russia wako umbali wa kilomita 200 kutoka mpaka wa Ukraine, na wanajeshi wengine 143,500 wa nchi hiyo wako umbali wa kilomita 400 ndani ya ardhi ya Russia.

Russia imekanusha madai ya nchi za Magharibi kwamba Moscow ina nia ya kuivamia Ukraine, ikiituhumu Marekani na washirika wake wa Ulaya kuwa zinazidisha mvutano kwa makusudi. Moscow pia imewasilisha mpango kwa NATO na Marekani, ikitaka kupewa dhamana na uhakikisho wa kuaminika kwamba Ukraine haitajiunga na NATO, na kwamba NATO haitaweka silaha za mashambulizi kwenye mipaka ya Russia. Matakwa haya ya Russia yamepingwa na NATO, Marekani na Umoja wa Ulaya. Moscow imekuwa ikipinga kujitanua kwa NATO upande wa Mashariki na uanachama wa nchi za kandokando yake hususan Ukraine katika shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi; na maafisa wakuu wa Russia wamewaonya viongozi wa Magharibi na Marekani juu ya madhara ya jambo hilo.

Baada ya kushika madaraka Viktor Yushchenko aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi kufuatia Mapinduzi ya Rangi ya Chungwa (Orange Revolution) mwaka 2004, Ukraine ilianza kuomba uanachama katika taasisi za Magharibi, ukiwemo Umoja wa Ulaya, na hasa NATO. Wamagharibi, ambao wamekuwa wakitaka kuidhoofisha Russia, waliunga mkono ombi hilo na kusaidia mikakati ya Ukraine ya kutaka kujitenga zaidi na Russia.

Hata hivyo, mgogoro wa Ukraine mwaka 2014, ambao kutokana na uingiliaji wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi, ulisababisha kupinduliwa kwa rais aliyechaguliwa na wananchi wa Ukraine, Viktor Yanukovych na hatimaye kuibuka kwa serikali nyingine yenye mielekeo ya Kimagharibi katika nchi ya Ulaya Mashariki, haukuwa na matunda ghairi ya kujitenga peninsula ya Crimea, vita vya wenyewe kwa wenyewe huko mashariki mwa Ukraine na hali mbaya ya kiuchumi.

Ted Galen Carpenter

Ted Galen Carpenter ambaye ni mtafiti katika Taasisi ya Quincy anasema: "Hatua ya Putin ya kuvamia na kuitwaa Crimea ulikuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, lakini hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Marekani na waitifaki wake wakuu ndani ya Umoja wa Ulaya kuwasaidia bila haya waandamanaji na kumuondoa madarakani Rais Viktor Yanukovych aliyekuwa amechaguliwa na wananchi."