Shule za msingi zaendelea kufungwa Uingereza kwa hofu ya ugaidi
Shule za msingi zilifungwa kwa siku ya tatu mfululizo nchini Uingereza jana Ijumaa kwa hofu ya kutokea vitendo vya kigaidi.
Gazeti la Independent la nchi hiyo limeripoti leo kuwa, shule 27 za Uingereza ziliendelea kufungwa jana baada ya kupigwa simu za vitisho vya kutegwa mabomu na kufanyika mashambulizi ya silaha katika shule hizo.
Mtu mmoja amepiga simu kadhaa na kutishia kuwa atawashambulia kwa risasi wanafunzi wa shule za msingi na kuwakata vichwa vyao huko Uingereza.
Polisi ya kupambana na ugaidi ya nchi hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa, vitisho hivyo havipasi kudharauliwa bali inabidi vipewe umuhimu mkubwa.
Raia wengi wa Uingereza wamekuwa wakijiunga na kundi la kigaidi la Daesh na kushiriki katika mauaji kwenye nchi mbalimbali duniani hasa katika nchi za Syria na Iraq. Hivi karibuni Daesh iliwataka wafuasi wake wafanye mashambulizi nchini Uingereza kama yale waliyofanya Paris, Ufaransa na Brussels, Ubelgiji.
Mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Daesh tarehe 13 Novemba 2015 mjini Paris, Ufaransa, yalipelekea 130 kuuawa na wengine 350 kujeruhiwa. Shambulizi jengine la kundi la Daesh lilitokea tarehe 22 Machi 2016 mjini Brussels, Ubelgiji na kuua watu 32.