DiCarlo: Vikwazo vya UN vimekuwa kibogoyo, havina tena taathira
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80194-dicarlo_vikwazo_vya_un_vimekuwa_kibogoyo_havina_tena_taathira
Wakati Umoja wa Mataifa ukiendelea kutumia vikwazo kama sera ya kuziadhibu nchi mbalimbali duniani, Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo katika Masuala ya Siasa na Kujenga Amani, Rosemary Anne DiCarlo amekiri kwamba utumiaji wa vikwazo hauna tena taathira kama ilivyokuwa hapo awali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2022 05:29 UTC
  • DiCarlo: Vikwazo vya UN vimekuwa kibogoyo, havina tena taathira

Wakati Umoja wa Mataifa ukiendelea kutumia vikwazo kama sera ya kuziadhibu nchi mbalimbali duniani, Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo katika Masuala ya Siasa na Kujenga Amani, Rosemary Anne DiCarlo amekiri kwamba utumiaji wa vikwazo hauna tena taathira kama ilivyokuwa hapo awali.

DiCarlo amesema kuwa, ili kuwa na ufanisi, vikwazo lazima viwe sehemu ya mkakati mpana wa kisiasa unaoambatana na mazungumzo ya kisiasa, upatanishi, ulinzi wa amani na kampeni maalumu ya kisiasa.

Katika miaka ya karibuni Umoja wa Mataifa umeziwekea vikwazo vikubwa nchi kadhaa kama Libya, Sudan, Mali na Yemen kwa kisingizio cha kuzishinikiza ili zisitishe vita na mapigano ya ndani. Japokuwa vikwazo hivyo vya UN vinalenga kubadili mienendo ya tawala na serikali za nchi husika kwa mujbu wa hati ya umoja huo, lakini utumiaji wa vikwazo hivyo dhidi ya nchi mbalimbali aghlabu umekuwa ukipuuza sheria na kanuni za kimataifa na misingi ya haki za binadamu. Mara nyingi vikwazo hivyo vya Umoja wa Mataifa vimekuwa vikitumiwa na madola makubwa na yenye nguvu hususan Marekani kama fimbo ya kuzikandamiza nchi zinazokaidi na kupinga sera zao. 

Katika mkondo huo huo wataalamu huru wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni walitoa taarifa wakisema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vinainyima idadi kubwa ya watu duniani haki ya kupata maendeleo na ustawi. Wataalamu hao walizitaka nchi zilizoweka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi nyingine kukomesha vikwazo hivyo au kuvipunguza hadi kiwango cha chini kabisa. 

Marekani na washirika wake wa Magharibi wanaounga mkono utumiaji wa vikwazo, katika miongo ya hivi karibuni wametumia fimbo hiyo kama chombo cha kuziadhibu nchi mbalimbali kwa kadiri kwamba hivi sasa Marekani inahesabiwa kuwa kinara wa kuweka vikwazo duniani na inaongoza kwa kutumia wenzo huo kwa ajili ya kutimiza malengo ya siasa zake za nje. Kuhusiana na hili, gazeti la The Hill limeripoti kuwa utumiaji wa vikwazo dhidi ya watu binafsi na nchi nyingine kama chombo cha sera za kigeni za Marekani umeongezeka mara kumi katika miongo miwili iliyopita. 

Takwimu zinaonesha kuwa, vikwazo vilivyowekwa na Wizara ya Fedha ya Merekani katika programu 37 tofauti dhidi ya watu binafsi na nchi mbalimbali vimeongezeka kutoka 912 mnamo 2000 hadi vikwazo 9,421 mwaka 2021. 

Washirika wa Marekani barani Ulaya pia hususan Uingereza wamekuwa wakishirikiana na serikali ya Washington katika sera hizo za uraibu wa vikwazo. Vikwazo hivyo vinatekelezwa kwa visingizio mbalimbali vya kisiasa, kibiashara, kiusalama na hata haki za binadamu dhidi ya nchi nyingine hususan zile zinazokataa kukubali sera za Marekani au zinazotambuliwa kuwa wapinzani wa Washington. 

Richard Neveu ambaye ni miongoni mwa wapangaji wa baadhi ya vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi nyingine anasema: "Madhumuni ya kuweka vikwazo ni kusababisha mashaka au tuseme maumivu na kukwamisha, kwa njia ambayo nchi inayolengwa na vikwazo ibadilishe mienendo yake."

Ingawa Umoja wa Mataifa na Marekani zinaendelea kutumia fimbo ya vikwazo kufikia malengo yao, lakini inaonekana kuwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa vimekuwa butu na kibogoyo na kupoteza taathira zake, kama alivyokiri Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Rosemary Anne DiCarlo.

Rosemary Anne DiCarlo

Kupungua kwa taathira ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kimsingi kunatokana na mataifa makubwa kutumia vibaya wenzo huo; na pili, kwa sababu ya hatua ya nchi zilizolengwa na vikwazo kubuni njia na mbinu mpya zaidi za kukwepa vikwazo hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, uraibu wa kuweka vikwazo wa baadhi ya nchi mfano Marekani, umeunyima Umoja wa Mataifa wenzo muhimu wa kuendeleza malengo yaliyoainishwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa.