Vikwazo vyenye wigo mpana vya Wamagharibi dhidi ya Russia
(last modified Fri, 25 Feb 2022 13:33:25 GMT )
Feb 25, 2022 13:33 UTC
  • Vikwazo vyenye wigo mpana vya Wamagharibi dhidi ya Russia

Baada ya Russia kuchukua uamuzi wa kuishambuulia kijeshi Ukraine, kambi ya magharibi imeonyesha radiamali katika fremu ya kuiwekea vikwazo Moscow ambapo kabla ya hapo madola hayo yalikuwa yameahidi kuchukua uamuzi huo.

Pamoja na hayo, kuna hitilafu za kimitazamo baina ya madola ya Ulaya kuhusiana na kuiwekea vikwazo vya kimsingi Russia.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamelaani vikali mashambulio ya Russia dhidi ya Ukraine mwishooni mwa kikao chao cha dharura kuhusiana na hujuma ya Russia dhidi ya Ukraine. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamewafikiana kwamba,  waiwekee vikwazo vikali sehemu ya sekta ya fedha, nishati na usafiri na uchukuzi ya Russia kutokana na taifa hilo kuishambulia kijeshi Ukraine. Aidha viongozi hao wameafikiana kuwa, waiwekee vikwazo Russia katika suala la usafirishaji bidhaa nje ya nchi, kudhamini fedha, sera za utoaji visa na baadhi ya viongozi wa Moscow. Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa amesema: Lengo la vikwazo hivyo hivi ni kuzima utendaji wa kiuchumi wa Russia, vikwazo ambavyo vitajumuisha uga wa masuala ya kibenki, tadibiri ya kifedha, usimamizi dhidi ya upelekaji nje ya nchi teknojia, sekta ya viwanda na usafirishhaji bidhaa nje ya nchi. Hata hivyo baadhi ya mataifa mengi ya kambi ya Magharibi kama Japan na Canada nayo yametangaza vikwazo vyenye wigo mpana dhidi ya Russia.

Marekani nayo kwa upande wake imetangaza orodha ya vikwazo vipya dhidi ya Russia kwa kisingizio cha Moscow kushambuliwa kijeshi Ukraine.

Kuhusiana na hilo, Rais Joe Biden wa Marekani amemtaja Rais Vladmir Putin wa Russia kuwa ni mvamizi na kuafikiana na suala la Russia kuwekewa vikwazo vizito pamoja na 'kifuruishi cha vikwazo chenye kuleta uharibifu' dhidi ya Moscow.

Rais Joe Biden wa Marekani

 

Biden amesema kuwa, benki nne za Russia ambazo hazikuorodheshwa katika awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo sasa zimejumuishwa katika vikwazo vya mara hii. Miongoni mwazo ni Benki ya VTB ambayo ni benki ya pili kwa ukubwa nchini Russia. Kuanzia leo fedha zote za Russia nchini Marekani zinazuiwa na uwezo wa Moscow katika kufanya biashara kwa kutumia sarafu za dola na Yen ya Japan unawekewa mbinyo na mpaka. Joe Biden amedai pia kuwa, vikwazo hivi vitakuwa na gharama kubwa kwa uchumi wa Russia katika wakati huo na muda baada ya muda.

Kwa kuzingatia kwamba, Russia ilikuwa imetabiri kabla ya hapo kwamba, itawekewa vikwazo na madola ya Magharibi, hivyo kwa kiwango kikubwa ilikuwa imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo hivyo. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetangaza kuwa, nchi hiyo itachukua maamuzi makali kama jibu dhidi ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi yake.

Suala lenye umuhimu katika vikwazo vipya vya madola ya Magharibi hususan Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia ni hili kwamba, kwa kuzingatia kuwa, mataifa ya Ulaya yanategemea gesi ya Russia hayana ubavu wa kuiwekea Moscow vikwazo vya kimsingi, vikali na vya kuumiza hususan dhidi ya  mfumo wa kimataifa wa mabadilishano ya kifedha baina ya benki ujulikanao kama SWIFT na ambao unadhibitiwa na Marekani.

 

Licha ya matakwa ya baadhi ya madola ya Ulaya kama Jamhuri ya Czech ya kufukuzwa Russia katika mfumo wa kimataifa wa mabadilishano ya kifedha baina ya benki unaojulikana kwa kimombo kama The Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication, (SWIFT), lakini mataifa makubwa ya Ulaya kama Ujerumani na Italia  yamepinga ombi hilo. Sababu ya hilo iko wazi.

Kwa kuzingatia kwamba, Russia inadhamini gesi ya Ulaya kwa takribani asilimia 40, kama Umoja wa Ulaya  utataka kuiwekea vikwazo Russia na kuizuia isipate fedha zake zinazopatikana kupitia mauzo ya gesi, katika mazingira hayo Moscow nayo itazuia usafirishaji wa gesi yake kuelekea Ulaya. Kwa kuzingatia kwamba, gesi ya Russia ina umuhimu mkubwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali kama ya vifaa vya kutia joto katika msimu wa baridi, uendeshaji wa mitambo ya umeme na matumizi katika sekta ya viwando, ndio maana mataifa muhimu ya Ulaya hayana ubavu wala uthubutu wa kuiwekea vikwazo Russia kama vya mfumo kimataifa wa mabadilishano ya kifedha baina ya benki, kwani kufanya hivyo kutaifanya Russia nayo ijibu mapigo kwa kuyakatia mataifa hayo nishati muhimu ya gesi wanayoitegemea.

Kwa kuzingatia kwamba, Benki Kuu ya Russia na kanali ya fedha ya nchi hiyo ingali iko wazi na inaweza kupokea fedha zinazotokana na mauzo ya gesi, kuwekewa vikwazo benki nyingine muhimu za Russia uamuzi uliotangazwa na Marekani inaonekana zaidi ni propaganda na mchezo tu wa kisiasa. Hatupaswi kusahau kwamba, vikwazo vipya vya Wamagharibi dhidi ya Russia ni upanga wa ncha mbili ambao matokeo yake mabaya yataukumba uchumi na sekta ya nishati ya mataifa mengi hususan Ulaya na Marekani. Hivi sasa vita dhidi ya Ukraine tayari vimepelekea kupanda bei ya mafuta, dhahabu na ngano katika soko la dunia.

Tags