Feb 26, 2022 02:39 UTC
  • Maandalizi ya mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran yamekamilika

Mkuu wa Idara ya masuala ya Qur'ani ya Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri amesema maandalizi ya mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani yanayofanyika kila mwaka mjini Tehran yamekamilika.

Majidi Mehr, ameeleza hayo katika mahojiano maalumu na chaneli ya televisheni ya Qur'ani na kufafanua kuwa, mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani tukufu yataanza siku ya Jumatatu ya tarehe 28 Februari na kuendelea hadi tarehe 5 Machi. Amesema, barua za mwaliko wa kushiriki katika mashindano hayo ya Qur'ani, tayari zimeshatumwa kwa nchi zaidi ya 90 kupitia ofisi za Vitengo vya Utamaduni, ofisi za uwakilishi wa kisiasa na Balozi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.

Majidi Mehr ameeleza pia kuwa, kwa mwaka wa pili, mashindano ya tartili, yaliyofanyika kwa majaribio kuanzia mwaka uliopita, yatafanyika tena kwa sura ya majaribio katika mashindano ya mwaka huu.

Mkuu wa Idara ya masuala ya Qur'ani ya Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri amebainisha kuwa, usomaji wa tajwidi, tartili na kuhifadhi Qur'ani yote kwa washiriki wanawake na wanaume ni miongoni mwa vitengo vya mashindano ya mwaka huu na akaongeza kwamba, sambamba na mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani tukufu, yatafanyika pia mashindano ya saba ya Qur'ani kwa wanafunzi wa skuli za nchi za Ulimwengu wa Kiislamu na vilevile mashindano ya tano ya Qur'ani katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa washiriki wenye ulemavu wa macho.../

 

 

Tags