Ufaransa na UK zalumbana kuhusu wakimbizi wa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81136-ufaransa_na_uk_zalumbana_kuhusu_wakimbizi_wa_ukraine
Wimbi la wakimbizi wa Ukraine ambalo linahesabiwa kuwa ni la kasi kubwa zaidi barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Duniani, limezitumbukiza nchi mbili za Ufaransa na Uingereza katika vita vya maneno na malumbano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2022 23:08 UTC
  • Ufaransa na UK zalumbana kuhusu wakimbizi wa Ukraine

Wimbi la wakimbizi wa Ukraine ambalo linahesabiwa kuwa ni la kasi kubwa zaidi barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Duniani, limezitumbukiza nchi mbili za Ufaransa na Uingereza katika vita vya maneno na malumbano.

Jana Jumatatu, vyombo vya habari viliripoti kuwa, vita vya Ukraine vimesababisha watu zaidi ya milioni moja na laki tano kuwa wakimbizi katika kipindi cha siku 10 na kulifanya wimbi la wakimbizi hao kuwa kubwa zaidi barani Ulaya tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Uchochezi uliofanya hivi karibuni na nchi za Magharibi katika mipaka ya Russia, uliifanya Moscow ianzishe operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine hapo tarehe 24 Februari 2022 na kusababisha wimbi kubwa la wakimbizi.

Jana hiyo hiyo shirika la habari la Reuters lilitangaza kuwa, mzozo na vita vya maneno baina ya viongozi wa Uingereza na Ufaransa ni ugomvi wa karibuni zaidi wa kidiplomasia tangu Uingereza ilipojitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Ni mzozo unaohusiana na wakimbizi wa Ukraine waliokwama katika mji wa Calés wa kaskazini mwa Ufaransa.

Wakimbizi katika mji wa Calés wa kaskazini mwa Ufaransa

 

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Gérald Darmanin juzi Jumapili aliitaka Uingereza kutoiachia Ufaransa peke yake mzigo wa wakimbizi wa Ukraine. Alisema, serikali ya London inatumia kisingizio cha kukosa visa wala vitambulisho vinavyotakiwa, kuwazuia wakimbizi kuingia nchini Uingereza.

Naye waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, Priti Patel amejibu shutuma hizo za Ufaransa na kusema kuwa, Uingereza imechukua hatua nyingi muhimu za kuwasaidia na kuwapokea wakimbizi wa Ukraine na kuhakikisha wanaungana na familia zao nchini Uingereza.