Maelfu waandamana Paris wakitaka Ufaransa iondoke NATO
Makumi ya maelfu ya watu wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, wakishinikiza nchi hiyo ijiondoe katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO).
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yenye jumbe zisemazo 'Uhuru' na 'Frexit' wamesikika wakipiga nara za "Tundoke NATO".
Wananchi wa Ufaransa wametumia jukwaa la maandamano hayo kulalamikia gharama ya juu ya maisha katika nchi hiyo ya Ulaya iliyogubikwa na kiwango cha kutisha cha mfumko wa bei za bidhaa.
Kadhalika waandamanaji hao wamemtaka Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ajiuzulu mara moja, huku wakiitaka serikali ya Paris iache kuipa Ukraine silaha.
Aidha waandamanaji hao wamelalamikia mgogoro wa nishati unaoisumbua nchi hiyo pamoja na nchi nyingine za Ulaya kutokana na vita vya Ukraine.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kusema Ulaya itakabiliwa na matatizo mengi katika kujidhaminia gesi wakati wa msimu wa baridi wa mwaka huu.
Russia ilikuwa ikidhamini takriban 40% ya gesi asilia kwa nchi za Umoja wa Ulaya, ambayo ilitumika kuzalisha umeme, joto la nyumba na kuendesha viwanda.
Hata hivyo baada ya Russia kusitisha upelekaji gesi asilia barani Ulaya kwa 75%, hivi sasa nchi za bara hilo zinakabiliwa na hali mbaya sana ya uhaba wa nishati.