Maandamano ya kutaka kufungwa kampuni za silaha za Israel yafanyika UK
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95820-maandamano_ya_kutaka_kufungwa_kampuni_za_silaha_za_israel_yafanyika_uk
Wanaharakati wa kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina wamefanya maandamano katika miji kadhaa ya Uingereza, kushinikiza kufungwa kwa mashirika ya kuzalisha silaha ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika nchi hiyo ya Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2023 07:46 UTC
  • Maandamano ya kutaka kufungwa kampuni za silaha za Israel yafanyika UK

Wanaharakati wa kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina wamefanya maandamano katika miji kadhaa ya Uingereza, kushinikiza kufungwa kwa mashirika ya kuzalisha silaha ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika nchi hiyo ya Ulaya.

Baadhi ya waandamanaji wamekusanyika nje ya kiwanda cha kuzalisha silaha cha Israel mjini Leicester, ambapo sanjari na kulaani jinai za kikatili za Israel dhidi ya Wapalestina, lakini wametaka kufungwa haraka kwa kampuni hiyo.

Waandamanaji hao wametoa makataa ya siku 30 ya kufungwa kwa kampuni hiyo, na iwapo haitafungwa muhula huo utakapomalizika, basi watachukua kile walichokiita 'hatua ya umma.'

Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji ya Glasgow na Brighton, ambapo waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera ya Palestina, walikuwa na mabango pia yenye orodha ya jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Kampuni hiyo ya Kizayuni mjini Leicester ya UAV Tactical Systems inamilikiwa na shirika kubwa la kuzalisha silaha la utawala haramu wa Israel la Elbit Systems. 

Harakati ya 'Palestine Action' inasema silaha hizo zinazozalishwa nchini Uingereza na kampuni ya Israel si tu zinatumika dhidi ya Wapalestina, lakini zinatumika pia kuwaua, kuwakandamiza na kudhumu watu wengine katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Uingereza pia imekuwa ikikosolewa kwa kuendelea kutuma silaha kwa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen.

Silaha hizo zinatumika kuua watu wa Yemen, na takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa maelfu ya raia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.