Siku ya Nakba na maandamano ya Wazungu
Mwaka huu, umri wa utawala haramu wa Israel umeingia katika mwaka wake wa 75, huku Wazayuni wakiendelea kufanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, wanawake na watoto wakiwa wahanga wakuu wa jinai hizo.
Kuuawa kinyama watoto wanne wa Kipalestina katika mashambulio yaliyofanywa na Israel katika siku za karibuni katika Ukanda wa Gaza ni tukio la karibuni zaidi la jinai hizo za kusikitisha zinazotekelezwa na Wazayuni huku jamii ya kimataifa ikiwa imekaa kimya bila kuchukua hatua zozote za kisheria dhidi ya utawala huo wa kibaguzi.
Shirika la Kimataifa la Kutetea Watoto wa Palestina limetangaza katika ripoti yake ya karibuni kuwa idadi ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi na vikosi vya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds (Jerusalem) na Ukanda wa Gaza tangu mwanzoni mwa mwaka huu imefikia 24.
Tarehe 15 Mei 1948, ambayo inajulikana kwa jina la "Nakbat" katika historia ya Palestina, ni siku ambayo Wazayuni walivamia,kuua na kuwafukuza Wapalestina 750,000 katika miji yao na kuharibu takriban vijiji 530. Walowezi wa Kizayuni hata walichukua hatua ya kubadilisha majina asilia ya vijiji na miji hiyo na kuipa majina mapya ya Kiyahudi ili kurahisisha juhudi za kupora na kuwapa makazi Mayahudi katika maeneo hayo.
Siku ya Nakba sio tu ni nembo ya maafa yaliyowapata Wapalestina tangu mwaka huo, bali pia inawakilisha masaibu na matatizo ambayo yametwishwa taifa la Palestina katika miongo kadhaa iliyopita. Kwa hakika, "Siku ya Nakba" ni kisa cha msiba na maafa ya kibinadamu yaliyopelekea kuharibiwa sehemu kubwa ya misingi ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kisheria ya Wapalestina ili kuandaa uwanja wa kutangazwa uwepo wa utawala haramu.
Mauaji ya Wapalestina yanaendelea kufanywa na utawala wa kigaidi wa Israel katika hali ambayo siasa za jinai za utawala huo na kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina huku ukiua kinyama wanawake na watoto wao wasio na hatia, zimeibua hasira ya fikra za waliowengi duniani ambapo sasa taasisi nyingi za kiraia zinazishinikiza serikali mbalimbali duniani na kuzitaka kutouunga mkono utawala wa Kizayuni. 'Harakati ya Vikwazo' dhidi ya utawala wa Israel ambayo imekuwa ikifanya mikutano ya kuwaunga mkono Wapalestina, pamoja na kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala huo, ni miongoni mwa mashinikizo hayo.
Nabilah Munib, Katibu Mkuu wa Chama cha Umoja wa Kisoshalisti cha Morocco, anasema kuhusu suala hilo kwamba mapatano na Israel ni usaliti mkubwa unaoweza kufanywa na nchi ya Kiarabu dhidi ya mustakbali wa Palestina.
Mwaka huu pia na katika mkesha wa Siku ya Nakba, maandamano makubwa ya malalamiko na ya kutetea taifa la Palestina yamefanyika katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uingereza na Italia, ambapo washiriki wametaka kukomeshwa uungaji mkono wa serikali za Ulaya kwa utawala katili wa Israel.
Jim Curran, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Ireland, anasema kuhusu lengo la kushiriki kwake katika maandamano hayo mbele ya ubalozi wa Israel mjini London kwamba, shabaha yake ni kupinga vitendo vya kigaidi vya utawala ghasibu wa Israel ambao umekuwa ukilenga kambi za wakimbizi na maeneo mbalimbali ya Wapalestina katika mashambulio yake ya wiki chache zilizopita na kuwaua kwa umati watu wasio na hatia.
Jinai za Israel zinatilia shaka kivitendo nara za eti kutetea thamani za kibinadamu zinazotolewa mara kwa mara na nchi za Magharibi na kufichua sura halisi ya nchi hizo kuhusu suala zima la haki za binadamu. Maandamano yaliyofanywa karibuni na raia wa Uingereza mbele ya jengo la BBC yalifichua wazi mbele ya macho ya walimwengu, mchezo hatari unaofanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi katika kuunga mkono jinai za Israel, jambo ambalo sasa linapingwa na raia wengi wa Uingereza.