Jun 30, 2023 06:45 UTC
  • Ubaguzi wa taaluma nchini Uholanzi kutokana na hofu ya vikwazo vya Marekani

Kufuatia uamuzi wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Uholanzi kwamba kampuni ya nchi hiyo kwa jina ASML inaruhusiwa kukataa kuwaajiri wafanyakazi wake kwa msingi wa utaifa na uraia wao, kampuni hiyo yenye uhusiano mkubwa wa kibiashara na Marekani, siku ya jumatatu ilitangaza kuridhishwa na uamuzi huo uliotolewa kwa maslahi yake.

Kampuni ya ASML, iliyoko katika jiji la Feldhoven, Uholanzi, ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa vifaa vya kompyuta duniani, ambayo ina wafanyakazi zaidi ya elfu 31 kutoka mataifa 120 tofauti. Taasisi ya Haki za Binadamu ya Uholanzi ilithibitisha wiki hii kwamba kampuni hiyo inaruhusiwa kukataa maombi ya watafutaji ajira kutoka nchi za Iran, Syria, Cuba na Korea Kaskazini ambao wanaweza kupata teknolojia nyeti ya Marekani, hata kama kufanya hivyo kutakuwa kinyume na sheria za Uholanzi. Kufuatia kukataliwa maombi ya kuajiriwa mhandisi wa elektroniki kutoka Syria aliyekuwa katika hatua za mwisho za kuajiriwa na kampuni ya ASML, taasisi moja inayopinga ubaguzi yenye makao makuu yake katika jiji la Rotterdam, Uholanzi, iliwasilisha malalamiko dhidi ya taratibu za kutolewa ajiri za kampuni hiyo, ikisisitiza kuwa sheria za Uholanzi haziruhusu ubaguzi kwa msingi wa utaifa.

Lakini Taasisi ya Haki za Binadamu ya Uholanzi imepinga hoja hiyo na kuandika katika uamuzi wake kwamba: "Sheria zinazotolewa na viongozi wa Marekani wakati mwingine huwa na taathira nje ya mipaka ya nchi hiyo. Hata kama sheria hizo hazikubuniwa na wabunge wa Uholanzi, lakini kwa hakika zinalilazimu shirika la ASML kuzitekeleza." Katika kujibu malalamiko ya taasisi ya kupinga ubaguzi, ASML imedai kuwa kuajiri watu kutoka nchi zilizotajwa ni ukiukaji wa sheria za Marekani, jambo ambalo linaweza kusababisha hatari ya Marekani kuiwekea vikwazo kampuni hiyo na kusimamisha shughuli zake huko Marekani.

Iran imeweza kupiga hatua kubwa ya kitaaluma na kiteknolojia licha ya vikwazo vya nchi za Magharibi

Hatua ya ASML, ambayo bila shaka imetekelezwa kwa ushirikiano na msaada wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Uholanzi, ina maana ya kufanyika ubaguzi wa wazi wa kielimu dhidi ya raia wa baadhi ya nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani. Hatua hiyo mbali na kuwa inalenga kuzuia ajira na kuimarika viwango vya kielimu vya wataalamu kutoka nchi hizo nne, yaani Iran, Syria, Cuba na Korea Kaskazini, ni mfano wa wazi wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika kwa msingi wa utaifa na uraia wa watu wanaotaka kufanya kazi katika shirika hilo la Uholanzi, ambalo linajishughulisha na utengenezaji wa vifaa vya elektroniki. Kwa hakika, kuwa na uraia wa baadhi ya nchi zinazopinga utawala wa mabavu na ubeberu wa Marekani kunawafanya washirika wa Washington barani Ulaya ambao wanaogopa kuwekewa vikwazo na Marekani, kukataa kuwaajiri wataalamu na wasomi katika nyanja nyeti katika taasisi na makampuni yao yanayojishughulisha na masuala ya teknolojia ya kisasa.

Bila shaka, hii si mara ya kwanza kwa nchi za Magharibi kuzuia elimu au ajira kwa raia wa nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani. Miaka michache iliyopita, Norway ambayo inapatikana kaskazini mwa Ulaya na iliyo na uhusiano wa karibu na Washington, iliwazuia wanafunzi wa Iran kusoma katika ngazi za juu katika taaluma nyeti, katika hatua iliyokwenda sambamba na matakwa ya Marekani. Kuhusiana na hilo, mapema mwaka 2014, polisi wa Norway waliwafukuza wanafunzi 64 wa Kiirani waliokuwa wakisoma taaluma mbalimbali za juu katika vyuo vikuu vya nchi hiyo. Wanachuo wa Iran kusomea taaluma nyeti ilitangazwa kuwa sababu ya kuchukuliwa hatua hiyo na polisi wa Norway, ambapo ubalozi wa Norway mjini Tehran uliwaonya wanachuoa waliokusudia kusafiri nchini humo kwa ajili ya masomo kwamba kukubaliwa kwao kusoma baadhi ya masomo nyeti kungekuwa sababu ya kukataliwa maombi yao ya vibali vya kusafiri. Hata hivyo mwezi Mei 2016, Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway iliondoa marufuku iliyokuwa inawazuia wanafunzi wa Iran kujiunga na vyuo vikuu vya nchi hiyo kwa ajili ya kusomea taaluma zinazohusiana na nishati ya nyuklia.

Chuo cha masomo ya tiba na matibabu mjini Tehran

Pamoja na hayo, lakini bado kuna kila aina ya vikwazo na vizuizi katika nchi washirika na waitifaki  wa Marekani na hata ndani ya Marekani kwenyewe ambavyo vinawazuia raia wa baadhi ya nchi kusoma katika nyanja nyeti. Kuhusiana na hilo, Chuo Kikuu cha Jimbo la Massachusetts kilichopo katika mji wa Amherst, Marekani, mwezi Februari 2015, kilitoa notisi yenye kichwa kinachosomeka, 'Utaratibu wa Kujiunga Wanafunzi wa Iran' na kusema: "Kuanzia sasa, raia wa Iran wanaotaka kusoma katika Chuo cha Uhandisi (kusomea uhandisi wa kemia, uhandisi wa umeme na kompyuta, uhandisi wa mitambo na viwanda) na katika Chuo cha Sayansi (kinachojumuisha taaluma za fizikia, kemia, microbiolojia, uhandisi na sayansi ya polima) hawatakubaliwa kufanya hivyo." Mohsen Pak Ayin, mjumbe wa Baraza la Uongozi la Jumuiya ya Amani ya Kiislamu Ulimwenguni anasema: Vikwazo vya kielimu dhidi ya nchi zinazopinga ubeberu wa kimataifa, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni moja ya mifano ya wazi ya ubaguzi wa kielimu unaotekelezwa na mfumo wa ubeberu duniani.

Tags