Mar 19, 2024 02:36 UTC
  • Jumanne, 19 Machi, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 08 mwezi Ramadhani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 19 Machi 2024.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza.

Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki.

Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Alifariki dunia mwaka 1950.

Sir Norman Haworth

Katika siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, Frederic Joliot mwanafizikia na mwanakemia wa Kifaransa alizaliwa huko Paris. Baada ya kusoma masomo yake ya Chuo Kikuu alifanikiwa kuwa msaidizi wa Marie Curie mwanafizikia na mvumbuzi wa radiamu. Baadaye alimuoa binti ya Marie Curie ambapo akishirikiana mkewe walifanikiwa kugundua mpangilio mpya wa radiactive. Frederic Joliot aliaga dunia mwaka 1958.

Frederic Joliot

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 29 Esfand 1329 Hijria Shamsia, baada ya vuta nikuvute na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza na utawala kibaraka wa mfalme hapa nchini, hatimaye wabunge wa Bunge la Taifa na lile la Seneti walipitisha muswada wa kutaifisha sekta ya mafuta nchini.

Kupitishwa muswada huo ilikuwa hatua muhimu katika mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza. Kufuatia kupasishwa sheria hiyo, Muswadiq aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Iran kwa kuungwa mkono wa wananchi na viongozi wa kidini hasa Ayatullah Kashani.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba na kuwataka wananchi wa Iran wasifanye sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 ili kulalamikia hatua zisizo za kisheria za utawala wa kifalme wa Kipahlavi.

Nairuzi ni sherehe za kitaifa za Wairani ambazo hufanywa mwanzoni mwa mwaka mpya wa Hijria Shamsia. Katika kipindi chote cha mwaka 1341 Hijria Shamsia utawala wa kidikteta wa Shah ulichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha misingi yake na kuyaridhisha madola ya kigeni hususan Marekani. Imam Khomeini akiwa pamoja na maulama wengine wa Kiislamu aliitangaza sikukuu ya Nairuzi kuwa mambolezo ya umma ili kubatilisha propaganda za utawala wa Kipahlavi za kuhalalisha hatua zake za hiana.

Kwa muktadha huo, wananchi na viongozi wa kidini walifanya vikao vya maombolezo katika pembe mbalimbali za Iran. Ubunifu huu wa Imam Khomeini ulikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, katika siku ya pili ya sikukuu ya Nairuzi maafisa wa utawala wa Shah walishambulia mkusanyiko wa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) katika mji wa Qum waliokuwa wakifanya maombolezo na kuwauwa shahidi na kuwajeruhi baadhi yao.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95.

Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel. 

Louis de Broglie