Mar 20, 2024 02:35 UTC
  • Jumatano, Machi 20, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 09 Ramadhani 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Machi mwaka 2024 Milaadia.

Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1403 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz.

Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz.

Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama sikukuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Tarehe 20 Machi miaka 297 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84.

Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.

Isaac Newton

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamedani. Alikuwa miongoni mwa maulamaa na wanazuoni wakubwa wa karne ya 13 na 14 Hijria Qamaria nchini Iran na alisifika kwa kuwa na takwa na uchamungu.Baada ya kukamilisha masomo ya msingi na kati, Ayatullah Hamedani alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu na alianza kufunza na kueneza elimu baada ya kukamilisha masomo yake.

Vitabu vyake vimekusanywa katika majmui iliyopewa jina la 'Tadhkiratul Muttaqiin'. 

Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamedani

Katika siku kama hii ya leo miaka 99 iliyopita barua rasmi za serikali ya Iran zilianza kuandikwa kwa kutumia tarehe ya mwaka wa Hijria shamsia kufuatia azimio lililopasishwa na Bunge la Taifa.

Kwa utaratibu huo kalenda ya Iran ilibadilika kutoka mwaka wa Hijria Qamaria na kuwa Hijria Shamsia. Mwanzo wa miaka hiyo miwili ya Qamaria na Shamsia ni mmoja yaani hijra na tukio la kuhama Mtume (saw) kutoka Makka na kwenda Madina katika mwaka wa 13 baada ya kupewa utume (mwaka 622), lakini mwaka wa Qamaria unahesabiwa kwa kuzunguka mwezi mara 12 kandokando ya sayari ya dunia, na mwaka wa Shamsia unahesabiwa kwa dunia kuzunguka jua mara moja.

Kwa kuwa mwaka wa Hijria Shamsia una siku 365, kila mwaka huwa na siku 11 zaidi ya mwaka wa Hijria Qamaria ambao huwa na siku 354. 

Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji. Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011. 

Na siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, vikosi waitifaki wa Marekani na Uingereza waliishambulia kijeshi Iraq kwa kisingizio cha nchi hiyo kuzalisha silaha za mauaji ya umati.

Hatua hiyo ilichukuliwa licha ya malalamiko makubwa ya walimwengu. Kufuatia vita hivyo vya umwagaji damu, zaidi ya makombora 1000 ya cruise, maelfu ya mabomu na makumi ya maelfu ya mizinga na mabomu ya vishada yalimiminiwa wananchi wasio na hatia wa Iraq. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wa Kiiraqi waliuawa katika vita hivyo.

Aidha nyumba zisizo na idadi za Wairaqi, hospitali, taasisi za kiuchumi, kiutamaduni na misikiti ilibomolewa. 

 

Tags