Apr 16, 2024 02:12 UTC
  • Jumanne, 16 Aprili, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 7 Shawwal 1445 Hijria sawa na 16 Aprili 2024.

Siku kama hii ya leo miaka 1442 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. Mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislamu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, alizaliwa mjini Paris Anatole France, mwandishi na malenga wa Kifaransa. Tangu akiwa kijana alivutiwa na elimu ya fasihi na uandishi ambapo kutokana na kipawa alichokuwanacho akatokea kupata umashuhuri katika uga wa mashairi na fasihi. Anatole France ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu kinachoitwa 'Mfalme wa Sabai.' Mwaka 1914 Anatole France alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na kuandika kitabu alichokipa jina la 'Uasi wa Malaika' huku akifariki dunia mwaka 1924.

Anatole France

Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo Wazayuni waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya zamani ya askari wa Uingereza huko Palestina na kuua Wapalestina 90 na kujeruhi wengine wengi. Kwa upande mmoja, maafa hayo yalitokea wakati askari wa Uingereza walipokuwa wakiondoka katika kambi hiyo na kurejea nchini kwao; na kwa upande wa pili, Wazayuni walikuwa wameshadidisha mauaji hayo ya Wapalestina wasio na hatia kwa lengo la kuasisi dola haramu la Israel. Matokeo ya mauaji hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa Uingereza, ilikuwa kuuawa idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa Palestina na kutangazwa dola bandia la Israel mwezi mmoja baadaye. ***

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita ulitokea mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi na kusambaza moto kwenye mahema ya Mahujaji huko Mina kilomita 10 kutoka katika mji wa mtakatifu wa Makka. Mahujaji wasiopungua 343 walifariki dunia na wengine 1,290 kujeruhiwa katika tukio hilo. Aidha mahema yasiyopungua elfu sabini yaliteketea kwa moto huo. Hilo linahesabiwa kuwa tukio kubwa la pili la janga la moto kutokea wakati wa msimu wa Hija. Mnamo mwaka 1975, ulitokea moto mkubwa huko Mina nchini Saudi Arabia uliosababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji na wengine wengi kujeruhiwa. Kutokana na matukio hayo, Saudi Arabia ililazimika kuweka katika eneo la Mina, mahema yasiyoshika moto ili kuepusha ajali za moto. *

Mahema ya mahujaji Mina yakiteketea kwa moto

 

Tags