Jumatatu tarehe 17 Julai, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Shawwal 1438 Hijria sawa na Julai 17, 2017
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake. Baraza hilo liliundwa kwa mujibu wa kipengee namba moja cha Katiba ya Iran kwa shabaha ya kukinda sharia za Kiislamu na Katiba na kuhakikisha kwamba sheria zote zinazopasishwa hapa nchini hazipingani na viwili hivyo. Baraza hilo linaundwa na wataalamu 6 wa elimu ya fiqhi wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria wanaoteuliwa na Idara ya Mahakama na kupasishwa na Bunge. Kazi kuu ya baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zote zinazopasishwa na Bunge haziendi kinyume na Sheria za Uislamu.
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Kiislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.
Miaka 49 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya Wakurdi wapinzani, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.
Na miaka 1097 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (saw) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa usomaji mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha tungo kadhaa za mashairi.