Aug 14, 2017 03:31 UTC
  • Jumatatu 14 Agosti, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Dhulqaada 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 mwezi Agosti mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Agosti 2006, yalimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili. Mapigano hayo yaliyoanzishwa na utawala wa Israel tarehe 12 Juni 2006, yalikuwa na lengo la kuidhoofisha na hata kuisambaratisha harakati ya Hizbullah. Kusimama kidete kwa wapiganaji wa Hizbullah dhidi ya majeshi ya Israel, kulimfanya Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah apate uungaji mkono mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah askari wa Kizayuni ambao awali walikataa mpango wa kusitisha vita walilazimika kuukubali mpango huo na kurudi nyuma bila ya mafanikio yoyote.

Wapiganaji shupavu wa Hizbullah

Siku kama ya leo miaka miaka 61 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti 1954, aliaga dunia malenga na mwandishi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Bertolt Brecht. Brecht alizaliwa mwaka 1898 Miladia katika jimbo la Ugsbourg nchini Ujerumani. Malenga na mwandishi huyo wa Kijerumani alihitimu elimu ya juu katika fani masuala ya asilia (nature). Malenga huyo wa Kijerumani ameacha vitabu na picha ambazo nyingi zinaeleza kuhusu utawala wa Manazi na udhalimu waliokuwa wakiutenda. 

Bertolt Brecht

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, nchi ya Pakistan ilijitenga rasmi na India na kujitangazia uhuru wake. Dini tukufu ya Kiislamu iliingia Bara Hindi katika karne ya 8 na sehemu ya ardhi hiyo ambayo leo inajulikana kwa jina la Pakistan ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18. Chama cha Muslim League kikiongozwa na Muhammad Ali Jennah kilianzishwa mwaka 1906 kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu baada ya kuanza harakati za wananchi wa India dhidi ya mkoloni Mwingereza. Chama hicho kilifanikiwa kuwashawishi Waislamu wa India na hatimaye kiliunda nchi ya Pakistan.

Tarehe 14 Agosti miaka 72 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti mwaka 1945 Japan ilisalimu amri mbele ya vikosi vya Waitifaki. Kwa utaratibu huo vita vilivyokuwa vimeanza mwaka 1939 kwa mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya Poland vikafikia kikomo. Japan na Marekani ziliingia katika vita vikali Disemba mwaka 1941. Vita hivyo vilimalizika baada ya Marekani kushambulia miji ya Hiroshina na Nagasaki kwa mabomu ya nyuklia ambayo yaliua karibu watu laki mbili. Kusalimu amri huko kwa Japan kwa hakika kulihitimisha Vita vya Pili vya Dunia.

Japan ilisalimu amri katika Vita vya Pili vya Dunia

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Yunis Ardabili. Mwanazuoni huyo ni mtoto wa Sayyid Muhammad Taqi Musawi Ardebili. Baada ya kusoma masomo ya utangulizi na ya kati huko Ardebil alielekea katika mji wa Zanjan na kusoma masomo ya Fiqihi na Usuul kwa Akhund Mullah Qurbanali. Baadaye alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu na kusoma kwa walimu mahiri wa zama hizo. msomi huyo ameandika vitabu kadhaa vya fiqhi, usulul fiqhi na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Yunis Ardabili