Apr 28, 2018 18:01 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (53)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 53.

Kwa wale mnaofuatilia kipindi hiki kwa karibu, bila shaka mnakumbuka kuwa katika mifululizo kadhaa iliyopita tulizungumzia viwezeshaji na vikwamishaji vya kupatikana umoja na kuwa na sauti moja nchi za Kiislamu, ambapo tulieleza kwamba lengo tukufu la kuikomboa Palestina na Quds tukufu na kukabiliana na adui wa pamoja wa Waislamu wote yaani Israel, ni nukta ya pamoja ya kisiasa na kiusalama; na vilevile kuasisi soko la pamoja la Kiislamu ni nukta ya pamoja ya kiuchumi ambayo kutokana na uwezo mkubwa na fursa zilizonazo nchi zote za Kiislamu nukta mbili hizo zina nafasi kubwa ya kufanikisha ndoto ya kufikiwa umoja na mshikamano wa Waislamu wote duniani. Na kama nilivyokuahidini katika kipindi kilichopita, kuanzia kipindi chetu cha leo na vyengine kadhaa vitakavyofuatia, tutaizungumzia ile iliyokuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC ambayo nayo pia ni moja ya nembo na vielelezo vya kuwepo sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kufanya hivyo tutajaribu kuidurusu na kuipitia tena misingi na malengo ya kuasisiwa jumuiya hiyo na kuona ni kasoro na udhaifu gani ambao umeifanya jumuiya hiyo ishindwe kufanikisha lengo la kuwepo umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ni jumuiya ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa katika jumuiya za kiserikali, ikiwa na nchi 57 wanachama kutoka mabara manne ya dunia. Historia na chimbuko la kuasisiwa jumuiya hiyo inarejea mwanzo wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Ukweli ni kwamba kufuatia kuanza vita hivyo, zile zama za kufuatilia fikra za Umajimui wa Kiislamu, kwa kimombo Pan-Islamism, ambazo zilitilia mkazo pia ufufuaji wa Khilafa ya Kiislamu zilifikia tamati; na Ulimwengu wa Kiislamu, ukaingia kwenye zama na kipindi kipya cha maisha yake ya kisiasa. Mabadiliko ya kisiasa na kimataifa ya kipindi hicho, hasa baada ya kushindwa Waislamu katika vita vya mwaka 1948 na kuasisiwa utawala haramu wa Israel, kuundwa nchi ya Kiislamu ya Pakistan katika maeneo ya Waislamu ya ardhi ya India, kujitokeza fikra ya Utaifa, yaani Nationalism kama idiolojia na nguvu muhimu ya kisiasa na kuanza taratibu vuguvugu la kuondokana na Ukoloni na kujitawala mataifa mbalimbali, vyote hivyo viliacha taathira kubwa kwa fikra za kisiasa za Waislamu. Masuala hayo yalikuwa chachu iliyozifanya fikra na harakati zenye mielekeo ya Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu zijiwe na wazo la kuasisi kambi moja ya nchi za Kiislamu katika mfumo wa kimataifa uliokuwepo zama hizo.

 

Kutokana na hayo, ilipoingia nusu ya pili ya karne ya ishirini, viongozi wa nchi za Kiislamu, nao pia walihisi umuhimu na udharura wa kuasisi jumuiya ambayo itakuwa na uwezo wa kujenga umma umoja unaotokana na mjumuiko wa nchi zaidi ya 50 za Kiislamu; na badala ya mfarakano na utengano kuleta umoja na mshikamano baina yao, pamoja na kwamba hata kabla ya hapo pia hamu na irada ya kuasisi jumuiya itakayokuwa nembo ya umoja wa Kiislamu, ilikuwepo siku zote miongoni mwa Waislamu hususan wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu; na hata kuna wakati ambapo kwa hima ya viongozi wa nchi za Kiislamu ziliwahi kufanyika juhudi mbalimbali kwa madhumuni ya kuunda taasisi ya kuuunganusha umma wa Waislamu duniani na vilevile kukabiliana na vitisho vinavyowakabili. Kufanyika mikutano na makongamano kadhaa katika baadhi ya nchi za Kiislamu, ukiwemo mkutano wa Makka wa Juni 1924, mkutano wa Cairo, Misri wa mwezi Mei 1926, mkutano mwengine wa Makka wa Juni 1926, kongamano la Baitul Muqaddas la mwaka 1931, mkutano wa Geneva wa mwaka 1935, kongamano la mabunge ya ardhi za Waarabu na Waislamu kwa ajili ya kuihami Palestina, ambalo lilifanyika mjini Cairo, Misri Oktoba mwaka 1938 na vilevile mfululizo wa vikao vilivyofanyika katika miaka ya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, vyote hivyo vinaonyesha kuwa nchi za Kiislamu daima zimekuwa na hamu ya kuasisi jumuiya za kimataifa zenye utambulisho wa Kiislamu.

Pamoja na yote hayo, kitu ambacho kilikuwa chachu ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na hatimaye Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ni tukio la kuchomwa moto msikiti mtukufu wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu lililotokea mwaka 1969. Tukio hilo lililosababishwa na Myahudi mmoja mwenye taasubi liliamsha hasira na ghadhabu za Waislamu duniani. Utawala haramu wa Israel ulimtaja mtalii mmoja kutoka Australia kuwa ndiye aliyehusika na uchomaji moto msikiti wa Al Aqsa. Na katika kuendesha kesi ya mtalii huyo Muastralia, mahakama ya Israel ilidai kwamba wakati alipotenda kosa hilo alikuwa na matatizo ya akili; na kwa mujibu wa sheria za ndani za utawala huo wa Kizayuni hawezi kuhukumiwa kwa kupewa adhabu yoyote ile. Uamuzi huo uliwakasirisha mno Waislamu na kuwafanya viongozi wa mataifa yao walazimike kuitikia sauti za malalamiko ya wananchi wao kwa kuwafikishia walimwengu ujumbe wa ghadhabu za Waislamu hao.

 

Katika kipindi hicho, Saudia Arabia na Morocco zilikuwa miongoni mwa nchi zilizofanya jitihada kubwa kuhakikisha kinafanyika kikao cha kuchunguza na kujadili suala hilo; na hatimaye mnamo Septemba mwaka 1969 mkutano huo ukafanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat. Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na viongozi wa nchi 20 za Kiislamu, wawakilishi wa nchi washiriki walijadili ajenda tatu kuu ambazo ni kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa, kukaliwa kwa mabavu ardhi za Waarabu na Israel na hali ya mji wa Baitul Muqaddas.

Katika mkutano huo mwakilishi wa utawala wa zamani wa Iran wa ufalme wa Pahlavi na mwakilishi wa serikali ya Uturuki walianzisha mabishano kuhusu kupitishwa azimio la kuilaani Israel na kuiunga mkono Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO; hata hivyo kwa jitihada zilizofanywa na baadhi ya nchi, mkutano huo uliwafiki kuitishwa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi washiriki kwa ajili ya kufuatilia jinsi ya kutekeleza maazimio yaliyopitishwa na mkutano wa viongozi wa nchi hizo na vilevile kuasisiwa Sekretarieti itakayoupa kasi mchakato wa ushirikiano wa nchi wanachama. Katika kikao cha kwanza cha mawaziri wa mambo ya nje kilichofanyika mwezi Machi mwaka 1970, washiriki waliifanyia kazi ajenda ya kuasisi Sekretarieti ya kudumu; na mji wa Jeddah ukaamuliwa kuwa makao ya muda ya Sekretarieti hiyo hadi itakapokombolewa Quds tukufu na kuhamishiwa katika mji huo wa Palestina. Mkutano wa pili mawaziri wa mambo ya nje ulifanyika mjini Karachi, Pakistan, ambapo katika mkutano huo Waziri Mkuu wa Malaysia, Tunku Abdul Rahman alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa OIC na kutakiwa aandae rasimu ya hati ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na kuiwasilisha kwenye mkutano utakaofuatia kwa ajili ya kupitishwa. Jumuiya ya OIC iliasisiwa rasmi katika mkutano uliofuata wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama uliofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia tarehe 24 Machi mwaka 1972 ambapo hati rasmi ya jumuiya hiyo ilipitishwa.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena inshallah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 54 ya mfululizo huu.

Tags