Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (4) +SAUTI
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa uwezo na tawfiki ya Allah tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia. Maulamaa ambao kama alivyosema Imam Ali bin Abi Twalib (as) kukaa nao huwa chimbuko la baraka.
Anasema: Keti na Maulamaa ili elimu yako iongezeke, adabu yako iwe njema na roho yako iwe safi. Katika vipindi vyetu viwili vilivyotangulia tulimzungumzia Abu Ja'far Muhammad ibn Ya'qub ibn Ishaq mashuhuri kwa jina la Sheikh Kulayni, mchango wake kwa Uislamu pamoja na hazina na dafina ya vitabu vyake vyenye thamani kubwa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya nne ya mfululizo huu kitamzungumzia Abu Ja'far Muhammad ibn 'Ali ibn Babawayh al-Qummi, mashuhuri kwa jina la Sheikh Saduq, alimu na mwanazuoni wa Kiirani ambaye ni msomi, mtaalamu na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kishia baada ya Sheikh Kulayni. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Abu Ja'far Muhammad ibn 'Ali ibn Babawayh al-Qummi, mashuhuri kwa jina la Sheikh Saduq ni mmoja wa Maulamaa wakubwa katika historia ya Ushia ambaye alichomoza kama nyota katika mbingu ya kupokea hadithi na ufakihi katika mji wa Qum. Hiyo ilikuwa ni katika karne ya nne Hijria. Mazazi ya Sheikh Saduq yalisadifiana na kuanza kipindi Abu al-Qasim al-Husayn ibn Ruh Nawbakhti naibu na mwakilishi wa tatu wa Imam Mahdi. Sheikh Saduq alizaliwa katika familia mashuhuri kwa elimu iliyojulikana kwa jina la Babawayh ambapo kwa zaidi ya miaka 300 walitokea katika familia hiyo katikati mwa Iran Maulamaa wakubwa na watajika. Sheikh Saduq anahesabiwa kuwa shakhsia mkubwa wa familia hiyo. Baba yake alikuwa msomi mkubwa katika mji wa Qum na mwandishi mwenye hima na idili ya hali ya juu katika kipindi cha Ghaibat Sughra ya Imam Mahdi (atfs) ambapo ameandika vitabu zaidi ya 200.
Baba yake Sheikh Saduq hadi anafikisha umri wa miaka 50 hakuwa amejaaliwa kupata mtoto. Siku moja alikata shauri kumwandikia Imam Mahdi barua kupitia kwa naibu na mwakilishi wake maalumu akimtaka Imam wake huyo wa zama, amuombee dua ili apate mtoto. Imam Mahdi akambashiria mazazi ya watoto wawili wa kiume ambao watakuwa watu wa kheri na baraka.
Mmoja wa watoto hao ndiye Sheikh Saduq ambaye kutokana na mapenzi makubwa, hamu, shauku, akili na uwezo mkubwa wa ufahamu ambao haukuwa na kifani alijifunza elimu na kwa baraka za dua ya Imam Mahdi akaondokea kuwa mmoja wa walimu mahiri na wakubwa katika zama zake. Kitabu mashuhuri zaidi cha Sheikh Saduq ni "Man La Yahdhruh al-Faqih, moja ya vitabu mashuhuri vya Waislamu wa Kishia katika hadithi vinavyojulikana kama "Kutub al-Ar'baa".
Sheikh Saduq alianza kusoma masomo ya dini kwa baba yake akiwa na umri mdogo kabisa na kufanikiwa kumaliza masomo ya msingi ya kidini mahala alipozaliwa yaani katika mji wa Qum mahala walipokuwa wakipatikana wanazuoni na wapokezi wakubwa wa hadithi. Katika kipindi hicho Sheikh Saduq alionyesha hima na idili kubwa ya masomo. Haukupita muda kipaji chake kikaanza kudhihiri hasa kutokana na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo aliokuwa nao. Baada ya hapo alianza safari yake ndefu ya kielimu kwa kusafiri katika maeneo mbalimbali. Mapenzi makubwa aliyokuwa nayo ya kukusanya maneno yenye nuru ya Mtume (saw) na Maasumina (as) ndiyo yalimsukuma ahame kwao na kuanza kufanya safari. Alikwenda katika kila sehemu ambapo palikuweko mwalimu mahiri na mpokezi wa kuaminika wa hadithi.
Tunaweza kusema kuwa, hakuna sehemu iwe ya mashariki au magharibi ambayo Sheikh Saduq hakwenda na kusikiliza hadithi.
Miongoni mwa maeneo ambayo Sheikh Saduq alifanya safari ni Bukhara, Tus, Isfahan, Marvi, Balkh, Sarakhs, Samarqand, Ferghana, Neyshabur, Makka, Madina, Kufa na Baghdad.
Moja ya matukio muhimu katika kipindi cha uhai wa Sheikh Saduq ni kuingia madarakani ukoo wa Kiirani uliojulikana kama Ale Buye ambao ulikuwa mfuasi wa madhehebu ya Kishia. Utawala huu wa kifamilia ulitawala kuanzia mwaka 322 hadi 448 Hijria katika sehemu kubwa ya Iran, Iraq, Bara Arabu mpaka katika mipaka ya kaskazini mwa Sham. Utawala wa Ale Buye ulikuwa na nafasi muhimu katika kueneza fikihi na siasa katika kipindi cha Ghaiba na ulijulikana kama utawala wa kwanza wa Kishia katika zama za Ghaiba. Utawala huo ulikuwa ukiheshimu na kuthamini mno nafasi ya Maulamaa na ulikuwa ukitambua ulazima wa kutekeleza nadharia na fatuwa zao.
Sheikh Saduq alihajiri na kuelekea katika mji wa Rey kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa utawala wa Ale Buye na akiwa huko akawa akijishughulisha na kazi ya kufundisha fikihi na hadithi za Ahlul-Beiti (as) na kubakia huko hadi mwishoni mwa umri wake. Rukn al-Dawla, mtawala wa Ale Buye, alikuwa akimchukua Sheikh Saduq na kumkalisha kando yake katika kila kikao alichokuwa akienda, ili kwa njia hiyo aweze kunufaika na rai na mitazamo yake katika masuala mbalimbali.
Kipindi cha utawala wa Ale Buye, zilikuwa zama za ustawi wa kielimu na kiutamaduni ambapo maktaba na skuli mashuhuri zilijengwa na kuanzishwa katika mji wa Rey. Aidha katika zama za Ale Buye, mji wa Rey ulipata mageuzi ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kifikra na kufikia katika kilele cha ustawi na ufanisi. Kuweko wasomi na wanazuoni watajika kama Abu Ali Sina, Muhammad Ibn Zakariya al-Razi na Sheikh Saduq ni ishara ya wazi ya kuchanua kielimu mji wa Rey.
Kwa hakika, Abu Ja'far Muhammad ibn 'Ali ibn Babawayh al-Qummi, mashuhuri kwa jina la Sheikh Saduq anahesabiwa kuwa mwanazuoni aliyekuwa na hima kubwa miongoni mwa mwanazuoni wa Kiislamu ambapo ameandika na kualifu takribani vitabu 300 katika maudhui mbalimbali. Idadi hii yenye thamani ya vitabu hasa kwa kuzingatia suhula chache na mazingira yaliyokuwa yakitawala karne 11 zilizopita, ni ithbati tosha kwamba, ni kwa kiasi gani alikuwa na hima kubwa na juhudi zisizochoka.
Sheikh Saduq alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu mbalimbali za Kiislamu kama Usul, Fikihi, tafsiri, elimu ya utambuzi wa wapokezi wa hadithi na ufahamu wa hadithi. Moja ya kazi alizofanya Sheikh Saduq katika uga wa hadithi ni kuzikusanya na kuziweka hadithi katika mafungu kulingana na maudhui. Kabla ya Sheikh Saduq hilo halikuwa limefanyika ambapo hata leo hii pamoja na suhula nyingi zilizopo jambo hilo haliwezekani kufanywa na mtu mmoja, lakini Sheikh Saduq aliweza kulifanya hilo.
Baadhi ya vitabu vya Sheikh Saduq ni: Man Lā Yahḍuruhū al-Faqīh ambacho ni kitabu cha pili katika majimui ya Kutub al-Araba'a, Ilal al-Shara'i kinachozungumzia falsafa ya hukumu na sababu ya kuletwa kwake. Vitabu vingine ni Kamal Al-Din wa Tamam Al-Ni'mah. Kitabu hiki kinazungumzia kuthibitisha kiakili na hoja za nakili uwepo wa Imam wa Zama pamoja na Ghaiba yake kuwa ndefu. Vitabu vingine vya Sheikh Saduq ni: Kitab al-Tawhid, al-Khisal, al-Amali, Uyun Akhbar al-Ridha na Kitab Ithbat Wilayat Ali (as).
Wapenzi wasikilizaji muda nao naona umetupa mkono hivyo kwa leo sina budi kukomea hapa. Kipindi chetu kijacho kitaendelea kumzungumzia Sheikh Saduq pamoja na kitabu chake chenye thamani cha Man Lā Yahḍuruhū al-Faqīh. Basi hadi tutakakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.