Ijumaa tarehe 5 Juni 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 5 mwaka 2020
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita sawa na tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Juni, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliojawa na huzuni waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht az-Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran. Zaidi ya wananchi na Waislamu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini pamoja na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomein, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye kuelekea eneo la Behesht az-Zahra kwa ajili ya mazishi.
Miaka 16 iliyopita Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer. Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni. Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans. Mwaka 1970 aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter. Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza. Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa. Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi hizo tatu za Kiarabu na kuyashinda kikamilifu.
Na siku kama ya leo miaka 237 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani. Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier. Tangu alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya ndugu wawili Montgolfier kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa angani nalo katika siku kama hii ya leo. Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani.