Aug 08, 2024 12:47 UTC
  • Kuuawa Haniyeh; damu katika mishipa ya muqawama

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeonyesha kilele cha kukataa tamaa na kukwama baada ya miezi kumi ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Gaza kwa kumuuwa kigaidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas). 

Historia ya kuundwa taifa bandia la Israel inakwenda sambamba na uvamizi, kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Wapalestina na kuwa wakimbizi raia hao. Uvamizi wa kijeshi na mauaji dhidi ya Wapalestina vinaendelea hadi leo katika historia ya utawala huo ambao msingi wake ni ubaguzi wa rangi wa Wazayuni. Kutekeleza mauaji ya kigaidi ni moja ya nyenzo kuu zinazotumiwa na Wazayuni kufanikisha malengo yao haramu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni wanadhani kuwa, kwa kuwauwa kigaidi shakhsia na viongozi wa Muqawama na mapambano ya ukombozi wa Palestina wanaweza kusambaratisha vuguvugu na ari ya mapambano hayo.

Miezi 10 imepita sasa ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kuishambulia ardhi ya Gaza kwa aina mbalimbali za silaha na mabomu. Wapalestina elfu arobaini wameuawa shahidi na makumi ya maelfu kujeruhiwa katika mauaji ya kimbari ya Israel lakini Wazayuni hawajaweza kufanikisha malengo yao ya kuiangamiza Hamas. Wazayuni hao sasa wamemuuwa kigaidi Ismail Haniyeh, shakhsia mtajika wa mapambano ya Palestina ikiwa ni katika jitihada zao za kupanua vita na kutaka kujitoa katika hali ya mkwamo. Hii ni katika hali ambayo historia ya Palestina inaonesha kinyume na fikra za viongozi wa utawala wa kibaguzi wa Israel. Historia ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina inaonyesha kuwa Muqawama hauishii kwenye matukio kama mauaji ya Ismail Haniyeh. Katika vipindi na zama zote za mapambano yao, Wapalestina wameshuhudia maajenti wa Israel wakiwauwa shahidi viongozi wao iwe ni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu au katika maeneo mengine ya dunia lakini mauajii hayo hayajafua dafu na mapambano ya ukombozi bado yanaendelea. *********                                                    ********

Kuuliwa shahidi Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas katika mji mkuu wa Iran, Tehran, huenda kukatambuliwa kimakosa kuwa ni pigo kwa kundi hili la kisiasa. Tangu Oktoba 7 mwaka jana hadi sasa Wapalestina wanaendeleza mapambano dhidi ya Israel katika vita visivyo na mlingano, hata hivyo viongozi wa Israel wanajua vyema kwamba abadan hawawezi kuwapigisha magoti Wapalestina ili kuachana na mapambano ya ukombozi. Vita hivyo visivyo na mlingano katika ardhi na mipaka iliyofungwa ya Gaza vimewasababishia Wapalestina hasara na maafa makubwa ya kiroho na kimaada, lakini kile kilicholikatisha tamaa jeshi  la serikali bandia ya Israel linalojizatiti kwa silaha za kisasa zaidi ni kutosalimu amri raia wa Palestina mkabala wa maghasibu Wazayuni  ambao wamelenga ardhi na utambulisho wa kitaifa wa Palestina. Kwa msingi huo Israel inakabiliwa na chuki na hasira ya jamii ya kimataifa inayopinga mauaji yanayofanywa na Wazayuni huko Gaza. Wazayuni hawajatimiza malengo yao ya kistratejia licha ya jinai zote hizo dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Kipalestina. Kwa kutekeleza oparesheni za kigaidi, viongozi wenye misimamo mikali wa Israel wanatumai kuwa watafanikiwa kuwakatisha tamaa Wapalestina ili wasiunge mkono muqawama na mapambano yao ya ukombozi, lakini tajiriba na historia vinathibitisha kinyume chake.****** 

Utawala wa Kizayuni hadi sasa haujatimiza hata moja kati ya malengo yake makuu yaani kusambaratisha mapambano ya ukombozi ya Hamas na kukomboa mateka wake baada ya miezi kumi ya mauaji ya kikatili katika Ukanda wa Gaza na katika Ukingo wa Magharibi. Wazayuni wamevuka mistari yote myekundu katika silsila ya jinai zao za kiuwendawazimu magharibi mwa Asia. Lengo la utawala wa Kizayuni ni kuhuisha nguvu ya kujilinda ambayo ilipata kipigo katika Oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi kumi iliyopita, Israel  imeshindwa kurejesha uwezo iliokuwa nao kabla ya Oktoba 7, bali udhaifu na kukata tamaa kwa utawala huo mkabala wa Mhimili wa Muqawama umedhihirika zaidi na zaidi. Kiasi kwamba hata waitifaki wa utawala wa Kizayuni huko Marekani na barani Ulaya pia wamelazimika kudhihirisha undumakuwili katika kuukingia kifua na kuuhami utawala huo. Hii ni katika hali ambayo sauti za kupinga na kuulaani utawala wa Kizayuni zinasikika miongoni mwa washirika wa karibu wa Marekani. 

Katika  mazingira haya, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akiungwa mkono na serikali ya Marekani na zile za Ulaya, hayuko tayari kuheshimu mipaka na mistari yoyote myekundu katika kutenda jinai na kuwaua Wapalestina. Ismail Haniyeh hakuwa mwanasiasa aliyejificha, na shughuli zake za kidiplomasia na kisiasa zilikuwa wazi kikamilifu. Mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas amefanya safari nyingi nchini Iran na sehemu mbalimbali za dunia, na kwa msingi huo swali linaloulizwa ni kwamba, kwa nini auwawe wakati na mahali maalumu, hasa saa chache baada ya hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran? 

Kwa kumuua shahidi Haniyeh nchini Iran, serikali bandia ya Israel haikumlenga tu kiongozi huyo wa Hamas, bali pia imekiuka mamlaka ya kujitawala ya  Iran na kuvuka mistari yote myekundu ya kisiasa na kidiplomasia. Nukta nyingine muhimu ni kwamba, mauaji ya kigaidi dhidi ya Haniyeh yalifanyika baada ya ziara ya Netanyahu huko Marekani, na hotuba yake katika Congress iliyoshangiliwa na kipigiwa makofi na wawakilishi wa Marekani.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel anahitaji kuendeleza vita na kuibua chokochoko za kila aina katika nchi mbalimbali ili aweze kujikwamua katika kinamasi cha migogoro ya ndani na nje na kutokana na hofu aliyonayo ya kupandishwa kizimbani na kuswekwa jela kufuatia kesi za ufisadi zinazomkabili na kushindwa serikali yake kutabiri na kukabiliana na oparesheni ya kimbunga cha al Aqsa ya  Oktoba 7.                                          

 

Tags