Mar 21, 2021 03:19 UTC
  • Kikao cha Alaska na kukaririwa tuhuma za Marekani dhidi ya China

Kushadidi mpambano baina ya Marekani na China tangu baada ya Joe Biden kushika hatamu za uongozi kumezifanya pande hizo mbili kuitisha kikao cha ngazi za juu ambacho kilifanyika Alkhamisi iliyopita katika eneo la Anchorage kwenye jimbo la Alaska.

Kikao hicho kimejadili wasiwasi na hitilafu zilizopo na uwezekano wa kuzitafutia suluhisho. 

Serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani imeanza maungumzo ya kwanza kabisa ya moja kwa moja ya ya ngazi za juu na nchi mpinzani wake, China, huku ikiituhumu nchi hiyo kuwa inahatarisha mfumo wa kimataifa. Katika kikao hicho, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani, Jake Sullivan alimwambia Yang Jiechi ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Kamisheni Kuu ya Siasa za Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China kwamba: "Sisi hatutaki vita, lakini tunakaribisha ushindani mkubwa, na daima tutalinda misingi yetu, watu wetu na marafiki zetu." Vilevile Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken amemwambia mwenzake wa China, Wang Yi kwamba, Washington itajadili "wasiwasi wake mkubwa" kuhusu hatua za China huko Xinjiang, Hong Kong na Taiwan, na vilevile mashambulizi ya mtandaoni yanayofanywa dhidi ya Marekani. Blinken amedai kuwa, kila moja kati ya masuala hayo linatishia mfumo wa kaida zinazolinda usalama wa kimataifa.

Kwa upande wake, Yang Jiechi ameashiria mashinikizo ya Washington kwa nchi mbalimbali kwa kutumia mabavu na kusema: Marekani inatumia nguvu za kijeshi na uwezo wake wa kifedha kwa ajili ya kuzishinikiza nchi nyingine. Ameongeza kuwa, Marekani inahatarisha mustakbali wa biashara ya kimataifa kwa kutumia vibaya suala la usalama wake wa kitaifa. 

Inaonekana kuwa serikali ya Joe Biden imeamua kutumia sera ya hujuma dhidi ya wapinzani wakuu wa Marekani katika medani ya kimataifa yaani China na Russia. Kuhusiana na China, mbali na misimamo mikali ya viongozi wa sasa wa Washington, Marekani imechukua hatua kadhaa za kuiadhibu nchi hiyo na kuiwekea vikwazo vya aina mbalimbali. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuzifutia vibali kampuni kadhaa za teknolojia ya mawasiliano za Kichina zinazofanyakazi nchini Marekani, kuzisaili kampuni kadhaa za teknolojia ya habari za Kichina kwa kutumia kisingizio cha usalama wa kitaifa na kurefusha vikwazo dhidi ya China kwa kile kinachodaiwa ni hali mbaya ya demokrasia huko Hong Kong. 

Rais Joe Biden wa Marekani  

Katika upande mwingine hatua za hivi karibuni za Marekani kama vikao vya pande nne vya wakuu wa Marekani, Japan, Australia na India ambavyo maudhui yake kuu ilikuwa kujadili tishio la China huko Mashariki mwa Asia, safari za maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Biden na mawasiliano ya Washington na Ulaya, India na washirika wake wengine, vinaonyesha kuwa, Marekani imekhitari sera za kuhujumu na mpambano dhidi ya Beijing. Hivyo, kwa kutilia maanani lugha iliyotumiwa na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani katika mazungumzo ya Alaska ambayo ilikabiliwa na jibu kali la China, inaonekana kuwa itakuwa vigumu kufikiwa mapatano ya kimsingi kuhusiana na hitilafu za pande hizo mbili katika mazungumzo hayo. Balozi wa China mjini Washington, Cui Tiankai alisema Jumatano iliyopita kwamba: "Marekani itakuwa katika njozi tupu kama inadhani kwamba maafisa wa ngazi za juu wa China wanakwenda kwenye theluji ya Alaska kwa ajili ya kulegeza misimamo na kusalimu amri." 

Balozi wa China mjini Washington, Cui Tiankai 

Ni wazi kuwa, mbali na tuhuma zinazokaririwa siku zote, wasiwasi mkubwa wa Washington kwa sasa ni kudhihiri China kama nguvu kubwa na nambari moja ya kiuchumi duniani katika miaka michache ijayo, na vilevile kuongezeka nguvu za kijeshi za China ambazo zitatoa changamoto kwa mahesabu ya kiusalama na nafasi ya kijadi ya Marekani katika eneo la Asia Mashariki. Kwa sababu hiyo Marekani inafanya kila liwezekanalo kuidhoofisha China. 

Kwa utaratibu huo inatarajiwa kuwa, katika kipindi cha utawala wa Biden, kutashuhudiwa awamu mpya ya mizozo baina ya Washington na Beijing, na uhusiano wa pande hizo mbili unatazamiwa kuzongwa na mivutano, hitilafu na patashika nyingi zaidi.     

Tags