IMF na Benki ya Dunia zafanya mikutano ya kwanza barani Afrika katika kipindi cha miaka 50
Mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) Kristalina Georgieva ametoa wito kwa mataifa tajiri kutoa msaada zaidi kwa nchi zinazoendelea zenye madeni, wakati akifungua mikutano ya kwanza ya IMF na Benki ya Dunia kufanywa katika ardhi ya Bara la Afrika katika kipindi cha miaka 50.
"Kuleta mikutano barani Afrika tena, ni hatua muhimu sana kiishara na kimaana," amesema Georgieva katika mkutano na wanachama wa mashirika ya kiraia.
Amebainisha kuwa bara hilo linapambana na matatizo "yanayofanana sana" kama miaka 50 iliyopita, ikiwa ni pamoja na mfumuko wa bei na "machafuko ya kisiasa katika maeneo mengi".
"Nchi nyingi ziko chini ya mzigo wa madeni ambayo yanaweza kuzikandamiza na tunatumai sana kwamba mikutano hii itakuwa mahali pa kujenga uaminifu zaidi miongoni mwa mataifa. Sote tunahitajiana," amesisitiza mkuu huyo wa IMF.
Wakopeshaji wa kimataifa kwa kawaida huwa wanajumuika pamoja kupitia mkutano wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu nje ya makao makuu yao Washington kila baada ya miaka mitatu. Marrakesh ilipaswa kuandaa mkutano huo mnamo mwaka 2021, lakini uliahirishwa mara mbili kwa sababu ya janga la Covid-19.