Machafuko mapya yaibuka CAR, wengi wakimbia makazi yao
Machafuko mapya yameibuka Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuwalazimu maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika nchi jirani za Chad na Cameroon.
Kwa mujibu wa Tume ya Kuwahudumia Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNCHR, watu walianza kukimbia makazi yao Juni 12 wakati mapigano yalipoanza baina ya wafugaji na wakulima katika mji wa Ngaoundaye, eneo la Ouham pende.
Katika taarifa, UNHCR imesema imewasajili wakimbizi 5,643 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati waliofika nchini Chad na wengine 555 walioingia Cameroon.
Tayari UNCHR inatoa misaada kwa wakimbizi 67,000 wa CAR walioke Chad na wengine 260,000 walioko nchini Cameroon huku wengine 415,000 wakiwa wakimbizi ndani ya nchi.
Mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ulishadidi zaidi mnamo Machi mwaka 2013, baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozize na waasi wa muungano wa Seleka.
Mgogoro huo ulifuatiwa na mauaji makubwa, ambayo waathiriwa wake wengi walikuwa Waislamu. Kundi la Kikristo la Anti-Balaka limekuwa likiendesha operesheni za wazi za mauaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Kulengwa Waislamu na mashambulio ya kundi la Kikristo na kigaidi la Anti-Balaka kumewafanya Waislamu wengi wa nchi hiyo waikimbie nchi na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani.