Mar 09, 2024 07:35 UTC
  • Juhudi za Afrika Kusini za mashinikizo zaidi ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni

Kufuatia kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, Afrika Kusini imewasilisha ombi la dharura katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ikiitaka korti hiyo ya Umoja wa Mataifa ichukue hatua zaidi za dharura dhidi ya Israel, ikisisitiza kuwa utawala huo wa Kizayuni umeendelea kupuuza amri iliyotolewa na chombo hicho cha sheria.

Vincent Magwenya, Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini ameiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, lengo la nchi hiyo ya Kiafrika la kuwasilisha ombi jipya katika mahakama ya ICJ ni kuzuia baa la njaa linaloukodolea macho Ukanda wa Gaza, sanjari na kutaka kudhaminiwa usalama na afya ya wakazi milioni 2.3 wa eneo hilo lililozingirwa. Katika faili hilo lililowasilishwa siku ya Jumatano, Afrika Kusini imeiasa ICJ ichukue hatua za dharura za kuzuia janga kubwa la kibinadamu huko Gaza, ikisisitiza kuwa Wapalestina wa Gaza wako katika hatari kubwa ya kufa njaa.

Taarifa ya Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa: Watu wa Gaza hawawezi kuvumilia tena. Tishio la baa la njaa sasa lipo wazi. ICJ inapasa kuchukua hatua sasa hivi ili kuzuia janga kubwa la kibinadamu kwa kuhakikisha kuwa haki za msingi zilizoainishwa kwenye Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari zinalindwa.

Vincent Magwenya

Afrika Kusini imeiambia Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuwa, watoto zaidi ya milioni moja wa Gaza wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa, na kwamba chombo hicho cha Umoja wa Mataifa kinapasa kuchukua hatua zaidi kuizuia Israel kupanua operesheni zake za kijeshi katika ukanda huo ulio chini ya mzingiro wa kibaguzi.

Kuhusiana na hilo, Michael Fakhri, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula sambamba na kutahadharisha kuhusu hali mbaya ya baa la njaa huko Gaza amesema: Israel inataka kuwaadhibu Wapalestina wote. Haya ni "mauaji ya kimbari". Kiwango hiki cha njaa hakijawahi kutokea huko Gaza. Watu wa Gaza wanakabiliwa na ghasia za muda mrefu, za polepole na zenye uchungu.

Ijapokuwa maafisa mbalimbali wa Umoja wa Mataifa na nchi nyingi wametoa radiamali kuhusiana na kukabiliwa na njaa ya watu wa Gaza na kutoa wito wa kubuniwa njia salama za kuwasaidia wananchi wa Palestina, lakini Israel inaendeleza jinai zake kwa uungaji mkono wa Marekani na nchi za Magharibi.

Kuhusiana na suala hilo, Afrika Kusini ambayo hapo awali iliwasilisha shauri la mashtaka dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikiutuhumu kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, kwa mara nyingine tena ilisisitiza juu ya udharura wa kuchukuliwa hatua na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ili kuhakikisha kunazuiwa mauaji zaidi ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Tangu wiki za kwanza za mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, Afrika Kusini imekuwa ikiituhumu Israel kuwa ni utawala wa ubaguzi wa rangi "apartheid" na mauaji ya halaiki huko Gaza na mbali na kuishtaki Israel, imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kusimamisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kutekelezwa usitishaji vita.

Mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni 

Ingawa hukumu ya awali ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ilitolewa kuhusu malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni, na kwa msingi wake, utawala wa Kizayuni ulitakiwa kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, lakini kivitendo Israel sio tu kwamba, inaendeleza mashambulizo dhidi ya Wapalestina, bali hivi sasa kwa kutekeleza sera ya njaa, imeanzisha rasmi mauaji ya kimbari kwa watu wa Gaza. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wakaazi wote wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa na hivi sasa takriban watu 378,000 wanataabika na kuteseka vibaya kwa njaa.

Gazeti la The Guardian limeandika katika muktadha huu: Hatua za Israel zinaonyesha kuwa, utawala huo ghasibu unakusudia kuwaangamiza Wapalestina kwa vile tu wao ni Wapalestina; kuwanyima watu chakula kwa makusudi ni jinai ya wazi ya kivita.

Hali mbaya ya Gaza imeiifanya jamii ya kimataifa kutoa wito wa kusitishwa vita katika ukanda wa Gaza. Nchi nyingi zimetoa wito wa kusitishwa mashambulizi ya Israel kwa kuanzisha kampeni mbalimbali, hata hivyo utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu Marekani wanapinga kutekelezwa usitishaji vita.

Marekani inaendelea kuitumia silaha Israel kwa ajili ya kuwaua watu wa Gaza na inatumia haki ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia kutolewa kwa azimio la kusitisha mapigano huko Gaza.

Hivi sasa kwa mara nyingine tena, Afrika Kusini imetoa wito wa kuhamasishwa nchi zote za dunia dhidi ya jinai za Israel na kuongezwa mashinikizo ya kimataifa hususan hatua kali ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ili kutekelezwa usitishaji vita na kuzuia mauaji ya kimbari ya Wapalestina kwa silaha ya njaa.

Wakazi wa Gaza wakabiliwa na njaa kutokana na vita vya kikatili vya Israel 

Pretoria imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kutoa amri ambayo kwa mujibu wake Israel itadhamini mara moja ufikishwaji a misaada na huduma zinazohitajika katika Ukanda wa Gaza.

Afrika Kusini inaamini kwamba, "hali ya dharura sana" inayotawala huko Gaza inahitaji Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuchukua uamuzi bila ya kuanza kuitisha vikao vipya, na jamii ya kimataifa nayo inapaswa kutoa ushirikiano unaohitajika katika uwanja huu.

Tags