UNSC yawasilisha azimio la kusitisha machafuko CAR
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewailisha azimio la kutaka kusimamishwa ghasia na machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati haraka iwezekanavyo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio lake hilo, limeyataka makundi yote yenye silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kusimamisha haraka machafuko na kuwaachia huru watoto wanaowashikilia bila ya kizuizi chochote.
Azimio la Baraza la Usalama limeeleza kuwa kurejeshwa amani na uthabiti na kusimamishwa mapigano na makundi yanayobeba silaha ni hitajio la sasa la Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa wale wote waliotenda jinai Jamhuri ya Afrika ya Kati wanapasa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Hii ni katika hali ambayo mauaji, unyanyasaji wa kijinsia, kuharibu mali za umma, mateso, kuwalazimisha raia kuyahama makazi yao na kuwatumia watoto kama wanajeshi; yote hayo yamekuwa masuala ya kawaida nchini humo.