Askri kadhaa wa Libya wauawa katika mapigano mapya Sirte
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12262-askri_kadhaa_wa_libya_wauawa_katika_mapigano_mapya_sirte
Mapigano mapya baina ya askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na genge la kigaidi la Daesh yamesababisha mauaji ya askari watano wa serikali katika mji wa Sirte, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2016 03:33 UTC
  • Askri kadhaa wa Libya wauawa katika mapigano mapya Sirte

Mapigano mapya baina ya askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na genge la kigaidi la Daesh yamesababisha mauaji ya askari watano wa serikali katika mji wa Sirte, kaskazini mwa nchi hiyo.

Duru za hospitali nchini humo zimeripoti kuwa, mbali na vifo hivyo, wanajeshi wengine 28 wa serikali wamepata majeraha mabaya katika mapigano hayo yaliyoanza jana Ijumaa karibu na eneo la Dolar, yapata kilomita 1.5 kusini magharibi mwa mji wa Sirte.

Wanajeshi wa Libya mjini Sirte

Haya yanajiri siku chache baada ya mapigano hayo katikati ya mji wa Sirte kusababisha kuuawa wanajeshi saba wa serikali na 49 wengine wengi kujeruhiwa. Jeshi la Libya linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilianzisha operesheni ya kuukomboa mji huo wa kistratajia kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh mwezi Mei mwaka huu, lakini vikosi vya serikali vimekuwa vikisonga mbele kwa mwendo wa kinyonga kutokana na kujaa mabomu ya kutegwa ardhini na vile vile kuweko magaidi wanaowalenga wanajeshi hao kwa risasi kutoka mbali.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh Libya

Mwaka mmoja uliopita, kundi la Daesh lilijipenyeza ndani ya Libya kutokana na kutokuweko serikali moja yenye nguvu nchini humo na kuteka baadhi ya maeneo ukiwemo mji wa bandari wa Sirte.