Serikali yazidi kuwabana wapinzani nchini Uganda
Huku siku chache tu zikiwa zimebakia hadi kufanyika uchaguzi mkuu wa Februari 18 nchini Uganda, polisi ya nchi hiyo leo imemtia mbaroni na baadaye kuwachia Daktari Kizza Besigye, kiongozi wa chama cha upinzani cha cha FDC. Besigye amekamatwa na polisi wakati alipokuwa anakwenda kwenye mkutano wa hadhara katika wilaya yenye shughuli nyingi, jijini Kampala.
Jeshi la Polisi limedai kuwa limemkamata Besigye baada ya kukaidi amri ya polisi ya kumtaka atumie barabara ya Mukwana kwa ajili ya kuelekea Kampala.
Besigye ni mmoja wa wagombea wanane wanaochuana na Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa Rais utakaofanyika siku chache zijazo.
Mgombea huyo urais wa tiketi ya FDC ameshikiliwa katika kituo cha polisi cha Barabara ya Kira kabla ya kuachiliwa huru.
Wafuasi wa Besigye wamesema kwamba, jeshi la polisi lilikusudia tangu zamani kumtia mbaroni mgombea huyo wa urais, na ndio maana wamempangia kutumia ngumu na ya mbali kwa makusudi wakijua kuwa hatoweza kuitumia ili wapate kumkamata.
Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo amesema, wamemtaka Besigye kutumia njia ambayo iko mbali sana na alikokuwa anakwenda. Polisi walianza kumfyatulia mabomu ya kutoa machozi yeye Besigye na viongozi wengine wawili wa upinzani.
Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Uganda amesema kuwa vyama vya siasa vimepigwa marufuku kufanya kampeni katika eneo hilo lenye msongamano mkubwa wa watu jijini Kampala.