Misri 'yakaribisha' kuwekwa Ikhwani katika orodha ya magaidi ya US
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135464-misri_'yakaribisha'_kuwekwa_ikhwani_katika_orodha_ya_magaidi_ya_us
Serikali ya Misri imepongeza hatua ya Marekani ya kuitambua rasmi Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni shirika la kigaidi.
(last modified 2026-01-14T06:22:10+00:00 )
Jan 14, 2026 06:22 UTC
  • Misri 'yakaribisha' kuwekwa Ikhwani katika orodha ya magaidi ya US

Serikali ya Misri imepongeza hatua ya Marekani ya kuitambua rasmi Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni shirika la kigaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imekaribisha uamuzi huo wa Washington na kuutaja kama "hatua muhimu," ikielezea kama kielelezo cha kile ilichokiita "hatari" ya kundi hilo kwa usalama wa kikanda na kimataifa. Marekani imeyaorodhesha rasmi mashirika tanzu ya Harakati ya Ikhawanul Muslimin nchini Misri, Lebanon, na Jordan kama makundi ya "kigaidi", na kuashiria kupamba moto kampeni ya Washington dhidi ya makundi ambayo inadai yanatishia maslahi ya Israel katika eneo la Asia Magharibi.

Cairo iliipiga marufuku Ikhwani tangu 2013, kufuatia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Misri, Mohamed Morsi, ambaye alishinda uchaguzi baada ya maandamano ya Uamsho wa Kiislamu kumpindua dikteta Hosni Mubarak.

Shirika tanzu la Ikhwani nchini Lebanon la al-Jamaa al-Islamiya pia limepinga tangazo hilo la Marekani, likisisitiza kwamba harakati hiyo ni shirika la kisiasa na kijamii lenye leseni, na linalofanya kazi kwa uwazi chini ya sheria za Lebanon kwa miongo kadhaa.

Utawala wa Trump umetaja uungaji mkono kwa Harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas katika Ukanda wa Gaza na "shughuli dhidi ya maslahi ya Israel" katika eneo hilo kama eti sababu za uamuzi wake. Novemba 2025, Trump alisaini dikrii na kuweka baadhi ya matawi ya kundi hilo la Kiislamu katika orodha ya "mashirika ya kigeni ya kigaidi".

Hatua hiyo kwa mara nyingine tena inaakisi wazi chuki aliyonayo Trump dhidi ya Uislamu na jamii ya Waislamu. Itakumbukwa kuwa rais huyo tayari ametia saini sheria ya kutoingia nchini Marekani raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu, kwa visingizio visivyo na msingi.