Ghana kuwarejesha nyumbani mamia ya raia walioko Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138322-ghana_kuwarejesha_nyumbani_mamia_ya_raia_walioko_afrika_kusini
Ghana imetangaza kwamba imeanzisha mchakato wa kuwahamisha takriban raia wake 300 kutoka Afrika Kusini kufuatia wimbi la maandamano dhidi ya wageni.
(last modified 2026-05-13T12:10:06+00:00 )
May 13, 2026 12:05 UTC
  • Ghana kuwarejesha nyumbani mamia ya raia walioko Afrika Kusini

Ghana imetangaza kwamba imeanzisha mchakato wa kuwahamisha takriban raia wake 300 kutoka Afrika Kusini kufuatia wimbi la maandamano dhidi ya wageni.

Rais John Dramani Mahama wa Ghana ameidhinisha hatua hiyo ili kuwasaidia watu ambao wamefuata ushauri na kusajiliwa na ubalozi wa nchi hiyo huko Pretoria.

Serikali ya Ghana inasema zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo walioko huko Afrika Kusini linalenga kuhakikisha usalama na ustawi wa raia huku kukiwa na ongezeko la mvutano na mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni.

Nigeria pia imeelezea wasiwasi wake baada ya mfululizo wa maandamano ya kupinga wahamiaji katika miji kadhaa kote Afrika Kusini, pamoja na madai ya kufanyika mashambulizi na vitisho dhidi ya raia wa kigeni.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amekana kwamba nchi hiyo ina chuki dhidi ya wageni, akisema mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni hayaakisi maoni ya serikali au jamii kwa ujumla.

Katika ujumbe wake wa kila wiki kwa taifa, Ramaphosa amelaani maandamano na vitendo vya uhalifu vinavyowalenga wageni, akionya kwamba hakuna mtu au kikundi chenye haki ya kuchukua sheria mikononi.

Katika siku za hivi karibuni makundi ya watu waliokuwa na mapanga, marungu na mikuki waliwashambulia raia wa kigeni katika mitaa ya miji ya Johannesburg na Cape Town wakiwatuhumu kuwa wanatumia fursa za kazi na ajira wa wazawa.

Haya yanakuja wakati ambapo Afrika Kusini, uchumi mkubwa zaidi wa viwanda barani Afrika, inakabiliwa na mashinikizo ya kijamii yanayoongezeka kutokana na ukosefu wa ajira wa karibu 30%, jambo ambalo limechangia kuongezeka chuki dhidi ya wahamiaji na katika baadhi ya matukio, vurugu na machafuko.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa idadi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini inazidi milioni tatu, ikiwa ni takriban asilimia 5.1 ya idadi ya watu. Wengi kati ya wageni hao wanatoka nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).