Watu wenye hasira washambulia kituo cha matibabu ya Ebola mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138546-watu_wenye_hasira_washambulia_kituo_cha_matibabu_ya_ebola_mashariki_mwa_kongo
Waandamanaji waliokuwa na hasira wameshambulia na kuchoma moto mahema kadhaa katika kituo cha matibabu ya Ebola katika jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wakijaribu kudai miili ya jamaa zao waliofariki dunia kwa ugonjwa huo.
(last modified 2026-05-22T14:41:33+00:00 )
May 22, 2026 14:38 UTC
  • Mahema ya wagonjwa wa Ebola yameshambuliwa Kongo
    Mahema ya wagonjwa wa Ebola yameshambuliwa Kongo

Waandamanaji waliokuwa na hasira wameshambulia na kuchoma moto mahema kadhaa katika kituo cha matibabu ya Ebola katika jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wakijaribu kudai miili ya jamaa zao waliofariki dunia kwa ugonjwa huo.

Vurugu hizo zilizuka katika hospitali ya Rwampara, nje kidogo ya  Bunia, makao makuu ya jimbo la Ituri, baada ya familia za watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa Ebola kutaka kupatiwa miili yao kwa ajili ya mazishi, zikipinga ripoti kuwa vifo hivyo vimesababishwa na ugonjwa wa Ebola.  

"Umati wa watu ulikusanyika nje ya hospitali, na waliponyimwa miili ya jamaa zao, walichoma moto mahema kadhaa ya wagonjwa wa Ebola, hali iliyosababisha polisi kunyunyiza gesi ya kutoa machozi na kufyatua  risasi za tahadhari," ameeleza Luc Malembe afisa wa serikali ya mtaa katika jimbo la Ituri alipozungumza na waandishi wa habari katika mji wa Rwampara.

Malembe ametoa wito wa kuelimishwa zaidi jamii ili watu wengi wawe na uelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola huko Ituri, jimbo ambalo tayari linakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama.

Ghasia hizi zinakumbusha matukio ya mwaka 2020 ambapo vituo kadhaa vya afya vilishambuliwa na makundi ya watu waliokuwa na silaha na raia wenye hasira kwa sababu ya kutokuwa na imani na wahudumu wa afya, wakati eneo la mashariki mwa Kongo lilipokumbwa na mlipuko wa Ebola.

Mlipuko wa ugonjwa huo ulitangazwa rasmi Mei 15 mwaka huu katika jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo.

Tangu wakati huo, mamlaka ya afya ya Kongo na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeripoti kuwa watu 600 wanashukiwa kuwa na maambukizi na 139 wameaga dunia hadi sasa.