Mkuu wa afya barani Afrika: Mlipuko wa Ebola unatishia nchi 10 zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138582-mkuu_wa_afya_barani_afrika_mlipuko_wa_ebola_unatishia_nchi_10_zaidi
Kituo cha Afya cha Umoja wa Afrika kimetahadharisha kuwa nchi kumi za Kiafrika ziko hatarini kuathiriwa na virusi vya Ebola, mbali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
(last modified 2026-05-24T03:23:21+00:00 )
May 24, 2026 03:21 UTC
  • Jean Kaseya, Mkuu wa Africa CDC
    Jean Kaseya, Mkuu wa Africa CDC

Kituo cha Afya cha Umoja wa Afrika kimetahadharisha kuwa nchi kumi za Kiafrika ziko hatarini kuathiriwa na virusi vya Ebola, mbali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.

Jean Kaseya Mkuu wa Kituo cha kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) amezitaja Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Zambaia kuwa nchi zilizo katika hatari ya kuathiriwa na ugonjwa wa Ebola.

Uganda imethibitisha wagonjwa watatu wa Ebola siku ya Jumamosi, na Shirika la Msalaba Mwekundu limeeleza kuwa wafanyakazi watatu wa kujitolea wa sekta ya afya wamepoteza maisha baada ya kuambukizwa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa homa ya Ebola inayosababisha kuvuja damu kuwa dharura ya kimataifa.

Inafaa kuashiria hapa kuwa ugonjwa wa Ebola umeuawa watu elfu 15 barani Afrika katika kipindi cha nusu karne iliyopita.

Shirika la Afya Duniani siku ya Ijumaa lilitangaza kuwa hatari ya maambukizi ya virusi vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni ya kiwango cha juu sana.