Mkutano wa India na Afrika waahirishwa kutokana na mlipuko wa Ebola
-
Ebola yashika kasi Afrika
Umoja wa Afrika (AU) umekubaliana na India kuahirisha mkutano uliopangwa kufanyika New Delhi kutokana na hofu ya kuenea mlipuko wa Ebola ulioua zaidi ya watu 160 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na mtu mmoja nchini Uganda jirani.
Mkutano wa nne wa Viongozi wa India na Afrika ulikuwa umepangwa kufanyika kuanzia Mei 28 hadi 31. Katika taarifa ya pamoja, India na AU zimesema zimejadiliana kuhusu “hali ya afya inayoendelea kubadilika” katika baadhi ya maeneo ya bara hilo, na kukubaliana kuwa itakuwa “busara” kuufanya mkutano huo tarehe ya baadaye.
India pia imeeleza “mshikamano wake kwa watu na serikali za Afrika,” na kusema iko tayari kuunga mkono juhudi za Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) katika kukabiliana na mgogoro wa Ebola.
Uahirishaji huu unakuja wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa mlipuko kirusi aina ya Bundibugyo cha Ebola katika mashariki mwa DRC na Uganda ni dharura ya afya ya umma duniani. WHO imetuma zaidi ya wataalamu 35 na waokoaji wa awali kwenda eneo husika.
Mamlaka za DRC zilitangaza mlipuko huo Mei 15—ikiwa ni janga la 17 la Ebola kuripotiwa nchini humo tangu virusi hivyo vilipotambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976. Hadi sasa, maafisa wameripoti zaidi ya kesi 670 zinazoshukiwa na zaidi ya vifo 160 vinavyoshukiwa, hasa katika maeneo ya Ituri na North Kivu. Kesi mpya pia zinaibuka South Kivu, ambako wapiganaji wa M23 wametwaa maeneo wakati mapigano mapya yakichacha dhidi ya serikali.
Aina ya Bundibugyo ya Ebola haina chanjo iliyosajiliwa wala tiba mahsusi, ingawa huduma za mapema za kusaidia mgonjwa zinaweza kuongeza uwezekano wa kupona.